Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi: Mataifa yanayopigania haki na uadilifu yazidi kujuana
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i94972-kiongozi_muadhamu_wa_mapinduzi_mataifa_yanayopigania_haki_na_uadilifu_yazidi_kujuana
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza katika salamu zake kwa mataifa yanayozungumza Kihispania juu ya kuzidi kujuana na kushirikiana mataifa yanayotetea haki na uadilifu.
(last modified 2026-07-31T06:29:55+00:00 )
Mar 11, 2023 04:31 UTC
  • Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi: Mataifa yanayopigania haki na uadilifu yazidi kujuana

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza katika salamu zake kwa mataifa yanayozungumza Kihispania juu ya kuzidi kujuana na kushirikiana mataifa yanayotetea haki na uadilifu.

Kwa mujibu wa tovuti ya habari ya Ofisi ya Hifadhi na Uchapishaji Athari za Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, salamu za Ayatullah Khamenei kwa mataifa yanayozungumza Kihispania zimefikishwa sambamba na kuzinduliwa toleo la Kihispania la kumbukumbu za Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu mjini Caracas, Venezuela.
Katika salamu na ujumbe wake huo wa maandishi Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, amesema: "itakuwa ni furaha kubwa sana kwangu kama nitakuwa nimeweza kuwasiliana nanyi wazungumzaji wa Kihispania kupitia kitabu hiki".
Ayatullah Khamenei ameongezea kwa kusema: "Hii ni sehemu fupi ya historia yangu. Ni uzuri ulioje kama sisi na nyinyi pamoja na mataifa yote yanayotetea haki na uadilifu tukazidi kujuana na kushirikiana. Namuomba Mungu akupeni bahati njema".
Kitabu cha "Seli Nambari 14" cha kumbukumbu za mapambano ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu

Uzinduzi wa toleo la Kihispania la kumbukumbu za Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu yenye jina la "Seli Nambari 14" umefanyika katika hafla maalumu huko Caracas, mji mkuu wa Venezuela, sambamba na maonyesho ya utamaduni ya Urafiki wa Iran na Venezuela, yaliyoandaliwa kwa hima ya wanaharakati wa kitamaduni wa Venezuela na wazungumzaji wa Kihispania kwa kuhudhuriwa na shakhsia wa kiutamaduni wa Iran na Venezuela.

Kitabu cha "Seli Nambari 14" kinasimulia kumbukumbu na wasifu wa Ayatullah Khamenei wakati wa mapambano dhidi ya utawala kibaraka wa mabeberu nchini Iran na kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu.../