Iran: Makubaliano yetu ya kubadilishana wafungwa na Marekani, yasitumiwe kisiasa
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i95046-iran_makubaliano_yetu_ya_kubadilishana_wafungwa_na_marekani_yasitumiwe_kisiasa
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa, kwa mtazamo wa Jamhuri ya Kiislamu, makubaliano ya kubadilishana wafungwa ni suala la kibinadamu kikamilifu na halipaswi kugeuzwa kuwa uwanja wa tamthilia za kisiasa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 12, 2023 23:28 UTC
  • Iran: Makubaliano yetu ya kubadilishana wafungwa na Marekani, yasitumiwe kisiasa

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa, kwa mtazamo wa Jamhuri ya Kiislamu, makubaliano ya kubadilishana wafungwa ni suala la kibinadamu kikamilifu na halipaswi kugeuzwa kuwa uwanja wa tamthilia za kisiasa.

Nasser Kan'ani amesema hayo usiku wa kuamkia leo Jumatatu kujibu hisia na majibu ya ajabu yaliyotolewa na Marekani kuhusu makubaliano ya kubadilishana wafungwa kati ya nchi hiyo na Jamhuri ya Kislamu ya Iran. 

Ametoa ufafanuzi wa suala hilo akisema, tangu mwezi Machi mwaka jana 2022, makubaliano ya maandishi ya kubadilishana wafungwa kati ya Iran na Marekani yalitiwa saini mbele ya mpatanishi fulani ambaye ni mwakilishi wa Marekani aliyetambulishwa rasmi na nchi hiyo. Pamoja na hayo, hadi hivi sasa makubaliano hayo yameshindwa kutekelezwa kutokana na ukwamishaji na visingizio vya kila aina vya serikali ya Marekani.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Hossein Amir-Abdollahian

 

Msemaji huyo wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran pia amesema, katika kipindi cha wiki za hivi karibuni pia, yalikuweko mabadilishano yasiyo ya moja kwa moja ya ujumbe baina ya Tehran na Washington kwa ajili ya kuhuisha na kusasisha makubaliano hayo.

Itakumbukwa kuwa, jana Jumapili, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Hossein Amir-Abdollahian alizungumzia makubaliano hayo ya kubadilishana wafungwa kati ya Iran na Marekani na kusema ni makubaliano mazuri. Alisema, kuna makubalinao mazuri yamefikiwa katika siku za hivi karibuni na kama masuala yote yatakwenda vizuri kwa upande wa Marekani, basi karibuni hivi kutafikiwa makubaliano rasmi kuhusu mabadishano hayo ya wafungwa.