Rais Raisi: Iran iligeuza vitisho, vikwazo kuwa fursa ya kustawi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i95070-rais_raisi_iran_iligeuza_vitisho_vikwazo_kuwa_fursa_ya_kustawi
Rais wa Iran Ebrahim Raisi amesema Jamhuri ya Kiislamu imegeuza vitisho vinavyotokana na vikwazo vya upande mmoja kuwa fursa ya kupata maendeleo makubwa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 13, 2023 09:26 UTC
  • Rais Raisi: Iran iligeuza vitisho, vikwazo kuwa fursa ya kustawi

Rais wa Iran Ebrahim Raisi amesema Jamhuri ya Kiislamu imegeuza vitisho vinavyotokana na vikwazo vya upande mmoja kuwa fursa ya kupata maendeleo makubwa.

Raisi aliyasema hayo wakati wa mkutano na waandishi wa habari na mwenzake wa Belarus Alexander Lukashenko baada ya kukutana katika Ikulu ya Saadabad mjini Tehran siku ya Jumatatu.

"Iran imeunda fursa kutokana na vikwazo vilivyotekelezwa kwa nchi, na tumepata maendeleo ya ajabu licha ya vitisho. Tuko tayari kushiriki uzoefu wetu na rafiki yetu Belarus,” Raisi alisema.

Amesema Iran na Belarus zinapinga kuegemea upande mmoja na hiyo ndiyo njia ya kuondosha vikwazo na kuleta maendeleo.

Lukashenko aliwasili Tehran Jumapili kwa mwaliko wa Rais Raisi.

Wakati wa mkutano wao wa pamoja na waandishi wa habari, Raisi pia alisema kuwa nchi hizo mbili zimekuwa na uhusiano kwa miongo mitatu na uhusiano kati yao umeongezeka wakati wa utawala wa sasa.

"Nchi zote mbili zimedhamiria kuboresha uhusiano na biashara zao," alisema. "Mahusiano ya kiuchumi kati ya Iran na Belarus hayalinganishwi na zamani."

Rais wa Iran Ebrahim Raisi (kulia) na Rais Alexander Lukashenko wa Belarus

Raisi pia alisema kuwa Iran na Belarus zimetia saini makubaliano katika sekta kama vile viwanda, migodi, biashara na kilimo leo, akielezea matumaini kwamba makubaliano hayo yanafungua njia ya kuboreshwa kwa uhusiano wa pande mbili.

"Tumedhamiria kukuza uhusiano wetu wa kikanda na Belarus na tulikuwa na mazungumzo yenye matunda na rais wa Belarus," Raisi alisema.

Ameongeza kuwa Iran na Belarus zinaweza kuimarisha ushirikiano wa pande mbili ndani ya fremu ya Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai (SCO) na Umoja wa Kiuchumi wa Eurasia (EAEU).

Lukashenko pia alisema: "Ni ukweli kwamba hakuna vikwazo na mashinikizo yanayoweza kuizuia Iran kuendelea na Iran yenye nguvu inaendelea kupiga hatua. Nyaraka nyingi zilisainiwa leo, ikiwa tutazitekeleza zote, tunaweza kuongeza biashara kati ya nchi hizi mbili hadi milioni 100.

"Vikwazo ni fursa na nchi mbili hazipaswi kukosa fursa hizi," rais wa Belarus aliongeza. Aidha Rais wa Belarus amesema:"Misimamo ya nchi hizo mbili ni sawa katika masuala ya kimataifa na kikanda, na zote zinataka ulimwengu wa haki na wenye pande nyingi." Lukashenko pia alimwalika rais wa Iran kutembelea Belarus.