Kanani: Iran iko tayari kuandaa mazingira ya kufikiwa amani nchini Ukraine
(last modified Tue, 14 Mar 2023 02:10:15 GMT )
Mar 14, 2023 02:10 UTC
  • Kanani: Iran iko tayari kuandaa mazingira ya kufikiwa amani nchini Ukraine

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema Tehran imekuwa ikipinga vita vya Ukraine tangu mwanzo, na kutangaza utayarifu wa Jamhuri ya Kiislamu wa kuandaa mazingira yanayofaa kwa ajili ya kufikiwa amani na kusimamishwa vita nchini Ukraine.

Akijibu swali kuhusu matukio ya Ukraine, Nasser Kanani, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema jana katika mkutano na waandishi wa habari kwamba Iran imekuwa ikipinga vita vya Ukraine tangu mwanzo na wala haiungi mkono upande wowote katika vita hivyo.

Kanani amesema kuwa Iran imekuwa ikitangaza mara kwa mara kwamba haijatoa silaha kwa upande wowote katika vita vya Ukraine, na kuongeza kuwa licha ya urafiki wake na Russia, lakini haiungi mkono kunyakuliwa maeneo ya nchi hiyo na kuwa iko tayari kuandaa mazingira ya kumalizwa vita hivyo.

Msemaji huyo wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran aidha ameashiria kuitwa balozi wa Iran katika Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Azerbaijan na kusema suala hilo limetokana na ndege ya Iran iliyokuwa ikifanya safari za kawaida za ufuatiliaji katika maeneo ya mpaka wa Iran na nchi hiyo. Amesema safari kama hizo zimekuwa zikifanyika katika eneo hilo katika siku za huko nyuma.

Nchi jirani za Iran na Azerbaijan

Amesisitiza ndege hiyo iliruka ndani ya mpaka na katika anga ya Iran, kwa umbali unaofaa kutoka mpaka wa Jamhuri ya Azerbaijan. Amefafanua kwamba iwapo kosa litatokea katika hali kama hiyo, rada na mifumo ya ulinzi kwa kawaida hutoa habari mapema. Amesema hakuna habari muhimu wala onyo lolote la rada au redio lililotolewa kuhusiana na safari ya ndege hiyo.

Msemaji huyo wa chombo cha diplomasia ya Iran amedokeza kwamba suala hilo lingeweza kuzungumzwa na kutatuliwa kirahisi na ubalozi pamoja na mwambata wa kijeshi wa Iran huko Baku. Kwa hivyo, hatua ya serikali ya Azerbaijan ya kumwita balozi wa Iran na kutangaza suala hilo katika vyombo vya habari haiwezi kuchukuliwa kuwa ilifanyika kwa nia njema iliyochukuliwa katika mfumo wa uhusiano na ujirani mwema.

Kanani pia ameashiria ushiriki wa Iran katika kikao kijacho kuhusu Syria mjini Moscow na kueleza kuwa, kuboresha uhusiano wa Syria na majirani zake ni moja ya vipaumbele muhimu vya Iran kwa sababu ujirani mwema kati ya Syria na nchi muhimu za eneo ikiwemo Uturuki, utachangia pakubwa katika kupatikana amani na utulivu katika nchi hiyo ya Kiarabu.