Iran yafungua kituo cha kisasa kabisa cha matibabu ya saratani Asia Magharibi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i95214-iran_yafungua_kituo_cha_kisasa_kabisa_cha_matibabu_ya_saratani_asia_magharibi
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Ebrahim Raisi amezindua kituo cha kisasa kabisa cha matibabu ya saratani mjini Tehran na akasema serikali yake inalenga kuboresha maisha ya wananchi kuondoa udhaifu uliokuwepo.
(last modified 2026-07-31T06:29:55+00:00 )
Mar 17, 2023 09:19 UTC
  • Iran yafungua kituo cha kisasa kabisa cha matibabu ya saratani Asia Magharibi

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Ebrahim Raisi amezindua kituo cha kisasa kabisa cha matibabu ya saratani mjini Tehran na akasema serikali yake inalenga kuboresha maisha ya wananchi kuondoa udhaifu uliokuwepo.

Ameyasema hayo Alhamisi alipofungua Kituo cha Kuzuia na Kutibu Saratani cha Barekat, mojawapo ya vituo vya kisasa kabisa katika uga wa kuzuia na kutibu saratani katika eneo la Asia Magharibi.

Raisi ameongeza kuwa kufunguliwa kwa kituo hicho ni "hatua muhimu katika mwelekeo wa kuondoa udhaifu nchini na kuhakikisha kuwa kuna vifaa vya hali ya juu kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya wananchi."

Kituo cha Kuzuia na Kutibu Saratani cha Barekat kimejengwa na Makao Makuu ya Utekelezaji wa Agizo la Imam Khomeini (MA). Kituo hicho cha kisasa kabisa kinatoa huduma zote zinazohusiana na uchunguzi, utambuzi na matibabu ya aina zote za saratani.

Raisi amepongeza juhudi za wataalamu na taasisi za afya kupunguza gharama huku pia akipongeza matumizi ya teknolojia ya kisasa katika kituo hicho kipya cha afya.

Rais amesema kituo hicho cha matibabu kinalenga kuondoa upungufu uliokuwepo na kutoa huduma za matibabu zenye ubora wa hali ya juu kwa gharama nafuu zaidi kwa wananchi huku akitoa wito wa kujengwa kwa vituo vya aina hiyo katika maeneo mengine nchini ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za matibabu kwa wananchi.

Rais Raisi akitembelea eneo moja la Kituo cha Kuzuia na Kutibu Saratani cha Barekat

Uzinduzi huo ulikuja wiki moja baada ya Rais Raisi  kufungua Hospitali ya Mahdi mjini Tehran ambayo imetajwa hospitali kubwa zaidi katika eneo la Asia Magharibi. Hospitali ya Mahdi ni mradi mkubwa zaidi wa matibabu nchini tangu Mapinduzi ya Kiislamu ya 1979, kwani  ina takriban vitanda 1,000 pamoja na vifaa vya matibabu vya hali ya juu ambavyo vitahudumia wagonjwa wa Iran na wa kigeni.

Iran imepata maendeleo makubwa katika nyanja ya tiba kwa miaka ya hivi karibuni, hususan katika maeneo ya utengenezaji wa dawa na vifaa vya matibabu pamoja na kutoa mafunzo kwa madaktari na wapasuaji katika vituo vya matibabu vya kisasa kote nchini.