Iran yalaani "unafiki' wa Ujerumani kuhusiana na silaha za nyuklia za Israel
(last modified Sat, 18 Mar 2023 04:08:16 GMT )
Mar 18, 2023 04:08 UTC
  • Iran yalaani

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani msimamo wa Ujerumani akisema ni wa "kinafiki" kuhusu mpango wa amani wa nyuklia wa Iran huku nchi hiyo ya Ulaya ikinyamazia kimya silaha za nyuklia za utawala wa Kizayuni wa Israel ambazo ni "tishio kwa eneo na dunia nzima".

Nasser Kana'ani ameeleza hayo katika taarifa aliyotoa kujibu matamshi ya Kansela Olaf Scholz wa Ujerumani aliyotoa katika mkutano na waandishi wa habari siku ya Alkhamisi akiwa pamoja na waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel Benjamin Netanyahu aliyeitembelea Ujerumani.

Kan'ani amesema, "inashangaza kwamba viongozi wa Ujerumani wanautaja mpango wa amani wa nyuklia wa Iran, ambao uko chini ya uangalizi mkali zaidi wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki, kuwa ni tishio lakini hawasemi hata neno moja kuhusu maghala makubwa ya silaha za nyuklia ya utawala bandia, ghasibu na usio na utu wa Kizayuni ambayo yanatishia amani na usalama wa eneo na dunia nzima".

Nasser Kan'ani

Katika mkutano huo na waandishi wa habari, Scholz alikariri madai ya nchi za Magharibi kwamba Iran inajaribu kutengeneza silaha za nyuklia na kusema kuwa Tehran haipaswi kuruhusiwa kuwa na nyuklia. Pia alisema Ujerumani inatoa kipaumbele kwa diplomasia kwa ajili ya kutatua suala hilo huku akidai pia kwamba Iran ni "tishio la kweli".

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amejibu madai hayo ya kizandiki ya Kansela wa Ujerumani kwa kusisitiza kwamba, nchi zenye misimamo huru na maoni ya umma ya walimwengu yamechoshwa na misimamo na mienendo hiyo yenye misingi ya undumakuwili; na siku hadi siku wanazidi kuwa na uhakika wa kufikia hitimisho kwamba, madai na shutuma za baadhi ya serikali za Magharibi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni za kizandiki na hazina itibari yoyote.../