Iran yawahukumu adhabu ya kifo magaidi wa shambulizi la Shah cheragh
Mahakama ya Iran imetoa hukumu ya kifo kwa watu wawili kwa kuhusika katika shambulio la kigaidi la Oktoba mwaka jana kwenye Harama ya mjukuu wa Mtume Muhammad (saw), Shah Cheragh, katika mji wa kusini wa Shiraz.
Mkuu wa Mahakama ya Mkoa wa Fars, Kazem Moussavi amesema kwamba wahusika wakuu wawili wa shambulio hilo la kigaidi wamepatikana na hatia ya kusaidia uharibifu duniani, uasi wa kutumia silaha na kutenda kuhujumu usalama wa taifa.
Amesema wawili hao walihusika moja kwa moja katika utayarishaji wa silaha, ununuzi wa vifaa na kutoa habari na mwongozo kwa mhusika mkuu wa shambulio la kigaidi dhidi ya Haram ya Shah Cheragh.
Kundi la kigaidi la Daesh lilidai kuhusika na shambulio hilo.
Mnamo Oktoba 26, 2022, gaidi aliyekuwa na silaha aliingia ndani ya haramu takatifu ya mjukuu huyo wa Mtume Muhammad (saw) katika mji wa Shiraz, na kuwaua Waislamu 15 waliokuwa wamekwenda eneo hilo kwa ajili ya kuzuru, wakiwemo wanawake na watoto, na kujeruhi wengine kadhaa kabla ya kukamatwa na askari usalama.
Gaidi huyo alifariki dunia baadaye akiwa hospitalini, kutokana na majeraha aliyoyapata wakati wa shambulio hilo lililoibua mshtuko mkubwa kote nchini Iran.
Washukiwa kadhaa walinaswa mara moja na takriban wiki mbili baadaye Wizara ya Usalama ya Iran ilitangaza kuwakamata magaidi 26 wa kitakfiri kwa kuhusika na shambulio hilo. Taarifa hiyo ilisema watu hao ni raia wa Jamhuri ya Azerbaijan, Tajikistan na Afghanistan, na hakuna hata mmoja wao ambaye ni raia wa Iran.
Moussavi amesema kwamba watu hao wawili waliohukumiwa kifo wamekiri kwamba walikuwa na mawasiliano na viongozi wa kundi la Daesh na wamesaidia kupanga shambulio hilo.
Afisa huyo wa mahakama ameongeza kuwa, washtakiwa wengine watatu katika kesi hiyo walihukumiwa kifungo cha miaka mitano, 15 na 25 kwa kuwa wanachama wa kundi la kigaidi la Daesh.