Mfalme Salman bin Abdul-Aziz amwalika Rais wa Iran kutembelea Saudi Arabia
Naibu Mkuu wa ofisi ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayohusika na masuala ya kisiasa amesema kuwa, Mfalme wa Saudia Salman bin Abdul-Aziz amemtumia barua ya mwaliko Rais Ibrahim Raisi ili akaitembelee Saudi Arabia.
Muhammad Jamshidi ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kiijamii wa twitter kwamba: Katika barua hiyo mfalme wa Saudia kwa Rais wa Iran amekaribisha kwa mikono miwili makubaliano yaliyofikiwa majuzi baina ya Iran na Saudia ya kuanzisha tena uhusiano wa kidiplomasia baina yao na kusema kuwa, anamwalika Rais Ebrahim Raisi kwa ziara rasmi nchini Saudia.
Aidha kwa mujibu wa duru za ofisi ya Rais wa Iran inayohusika na masuala ya kisiasa, Mfalme wa Saudia ametoa mwito katika barua yake hiyo juu ya kuimarishwa ushirikiano wa kiuchumi baina ya pande mbili.
Kwa upande wake Rais Ebrahim Raisi wa Iran amepokea mwaliko huo na kusisitiza kwamba, Iran iko tayari kuimarisha ushirikiano na Saudi Arabia.

Mwaliko wa Mfalme Salman kwa Rais wa Iran kuzuru Saudia unakuja chini ya siku kumi baada ya Riyadh na Tehran kufikia makubaliano ya kuanzisha tena uhusiano wa kidiplomasiia baina yao.
Makubaliano hayo yalifikiwa Ijumaa iliyopita katika mji mkuu wa China, Beijing, baada ya siku kadhaa za mazungumzo magumu kati ya Katibu wa Baraza Kuu la Usalama la Taifa la Iran (SNSC) Ali Shamkhani na mwenzake wa Saudia.
Kurejeshwa kwa uhusiano huo kulitangazwa rasmi katika taarifa ya pamoja ya Iran, Saudi Arabia na China Ijumaa iliyopita.
Saudi Arabia ilikata uhusiano wa kidiplomasia na Iran mnamo Januari 2016 baada ya waandamanaji wa Iran, waliokasirishwa na hatua ya Saudia kumnyonga kiongozi mashuhuri wa Kishia Sheikh Nimr kuvamia ubalozi wake mjini Tehran na ubalozi mdogo wa Riyadh mjini Mash'had.