Iran yapongeza misimamo ya Mauritania ya kuunga mkono taifa la Palestina
(last modified Wed, 05 Apr 2023 07:08:36 GMT )
Apr 05, 2023 07:08 UTC
  • Iran yapongeza misimamo ya Mauritania ya kuunga mkono taifa la Palestina

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amepongeza na kusifu misimamo ya serikali na wananchi wa Mauritania ya kuunga mkono malengo matukufu ya wananchi wa Palestina.

Hussein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema hayo katika mazungumzo yake hapa mjini Tehran na Dah Ould Sidi Ould Amar Taleb, Waziri wa Masuala ya Kidini wa Mauritania na kusifu pia hatua ya Mauritania ya kushiriki katika maonyesho ya kimataifa ya Qur'ani yanayofanyika hapa mjini Tehran.

Kwa upande wake Dah Ould Sidi Ould Amar Taleb, Waziri wa Masuala ya Kidini wa Mauritania ameonyesha kufurahishwa kwake na makubaliano yaliyofikiwa hivi karibuni baina ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na utawala wa Saudi Arabia yenye lengo la kuhuisha uhusiano wao wa kidiplomasia.

 

Waziri huyo wa Mauritania anayehusika na masuala ya Kiislamu amebainisha kwamba, makubaliano hayo ni kwa maslahi ya wananchi wa mataifa yote mawili, kwa eneo la Asia Magharibi na kwa mataifa yote ya Kiislamu.

Kadhalika, Dah Ould Sidi Ould Amar Taleb, Waziri wa Masuala ya Kiislamu wa Mauritania amepongeza na kusifu pia himaya na uungaji mkono wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa taifa la Palestina na kueleza bayana kwamba, kadhia ya Palestina siyo suala linalohusiana na wananchi wa Palestina tu, bali ni jambo la Umma wote wa Kiislamu na kwamba, siku zote Jamhuri ya Kiislamu imekuwa mstari wa mbele katika kadhia hii.

Tags