Uhuru katika hotuba ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu
Kongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza umuhimu wa uhuru na kusema kuwa uhuru una vipengee tofauti na unapaswa kuelekeza kwenye utukufu wa binadamu.
Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, ameyasema hayo katika mkutano wake na zaidi ya wanafunzi wa vyuo vikuu.
Uhuru ni miongoni mwa mambo ambayo madola ya Magharibi yameyavalia njuga na kuyatumia katika propaganda zao za kujipigia debe na kwa ajili ya mashinikizo dhidi ya nchi zisizofungamana na sera na mitazamo yao, kama vile Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Nembo kuu ya uhuru kwa mtazamo wa Magharibi ni ubinafsi na mambo ya anasa na ya kidunia. Katika nyanja za kisiasa pia Magharibi hukubali uhuru wa kiasi fulani usiopinga na maadili na kanuni zake na usiotoa changamoto kwa sera na siasa zake.
Ufafanuzi na maana hii ya uhuru haikubaliwi na Uislamu. Kwani sambamba na kutilia mkazo uhuru wa binadamu, Uislamu hautofautishi baina ya binadamu kwa msingi wa rangi, dini, mbari zao n.k. Katika mtazamo wa dini ya Kiislamu, uhuru unahusu pande mbili za kidunia na Akhera, na unapaswa kugusa mambo yote ya dunia na Akhera ya kiumbe huyo. Kutoa maana ya uhuru ndani ya mipaka ya maisha ya kimaada na kidunia pekee ni kuudhalilisha na kuudunisha uhuru. Kwa mtazamo wa dini ya Uislamu, lengo kuu la uhuru ni kumuinua juu mwanadamu, na sio kushusha hadhi yake na kuwa kiumbe mwili na matakwa na matamanio ya kimwili tu.
Kwa msingi huo, akihutubia mkutano wa wanafunzi wa vyuo vikuu, Kiongozi Muadhamu wa Mpinduzi ya Kiislamu amesema: "Uhuru ni jambo lenye umuhimu mkubwa sana. Sehemu muhimu zaidi ya nadharia ya uhuru katika Uislamu ni uhuru wa kuondoka kwenye tundu (mzingo) la umaada. Mtazamo wa kimaada unasema kwamba, siku moja ulizaliwa, unaishi kwa miaka michache, na baadaye utakufa, sote tutatoweka. Katika fremu hii ya mwili wa kimaada, wanakupa uhuru wa kiasi fulani; Uhuru wa kutimiza tamaa za kingono, uhuru wa hasira, uhuru wa kudhulumu, na aina nyingine kama hizi za uhuru; Huu sio uhuru. Uhuru halisi ni uhuru wa Uislamu. Uislamu hautufungii katika fremu na tundu hili la kimaada (mwili na matakwa yake). Unatwambia kuwa kufariki dunia sio mwisho wa mwanadamu bali ni mwanzo wa awamu nyingine mpya ambayo ndiyo asili na halisi. Unapoangalia kwa mtazamo huu, basi unaweza kukwea daraja za juu, na hakutakuwa na kikomo kwa harakati zako, kwa maendeleo yako, kwa ukamilifu wako; Huu ndio uhuru."
Suala jingine ni kuwa katika ulimwengu wa Magharibi, uhuru wa kisiasa na madai ya kutetea haki za binadamu huwa na maana hadi pale unapokuwa haujatoa changamoto kwa ushawishi wa kisiasa na kiutamaduni wa nchi za Magharibi duniani. Sera za kupiga vita Uislamu (islamophobia) na kumtukana na kumvunjia heshima Mtume muhammad (saw) na Qur'ani Tukufu na uungaji mkono wa serikali za nchi za Magharibi kwa vitendo hivyo ni mifano ya mienendo ya nchi za Magharibi, ambayo inaonyesha kwamba uhuru wa kisiasa katika jamii za Magharibi, kivitendaji, ni madai na propaganda tupu.
Kwa hakika, nchi za Magharibi hutumia uhuru eti wa kisiasa na pia haki za binadamu, wanazoziarifisha kulingana na uhuru wa watu binafsi, kama wenzo na fimbo ya kushinikiza nchi nyingine.
Katika mkutano wake na wanafunzi wa vyuo vikuu, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei amekutaja kujikomboa kutoka kwenye utumwa wa fikra mgando, kufifia, kubakia nyuma katika nyanja mbalimbali na chuki zisizo na maana, kujikomboa kutoka kwenye utumwa wa madola makubwa na kuondoka kwenye utumwa wa madikteta, kwamba kunakwenda sanjari na uhuru wa kibinafsi na uhuru wa imani na kujieleza, ambao unasisitizwa na kuungwa mkono na Uislamu.