Iran yalaani shambulio la kigaidi la Uganda lililoua zaidi ya watu 40
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amelaani vikali shambulio la kigaidi nchini Uganda lililouwa makumi ya wanafunzi katika shule moja ya sekondari Magharibi mwa nchi hiyo.
Nasser Kan'ani Chafi, msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, shambulio la kigaidi la kutisha nchini Uganda limezusha wahaka na wasiwasi mkubwa na kueleza kwamba, shambulio hili la kinyama kwa mara nyingine tena limeonyesha kuwa, uugaidi na uchupaji mipakka ni tishio la ulimwengu mzima.
Aongezeka kuwa, shambulio la kigaidi la Uganda dhidi ya wanafunzi kwa mara nyingine tena limethibitisha kwamba, kuna haja ya kuweko vita na mapambano athirifu sambamba na ushirikiano wa jamii ya kimataifa dhidi ugaidi.
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran sambamba na kutoa mkono wa pole na kutangaza kuwa pamoja na serikali na wananchi wa Uganda katika kipindi hiki kigumu cha majonzi hususan familia za wahanga wa shambulio hilo la kigaidi amesema kuwa, ana matumaini kwamba, kuweko mapambano ya kweli dhidi ya ugaidi na uchupaji mipaka kutayafanya maeneo mbalimbali ya dunia likiwemo bara la Afrika kushuhudia utulivu na amani.
Wakati huo huo, Uganda imeimarisha ulinzi na tayari imeanzisha msako mkubwa baada ya wanamgambo wenye silaha wa ADF wenye mfungamano na kundi la kigaidi ya Daesh (ISIS) kuwauwa watu wasiopungua 41; wengi wao wakiwa ni wanafunzi. Mauaji hayo yamefanyika katika maeneo ya Magharibi mwa Uganda karibu na mpaka na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.