Raisi: Muqawama umefichua kuwa Israel haina uwezo wa kujihami
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i99030-raisi_muqawama_umefichua_kuwa_israel_haina_uwezo_wa_kujihami
Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kambi ya muqawama imeanika njozi na uwezo bandia wa kujihami wa utawala wa Kizayuni wa Israel.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 21, 2023 00:15 UTC
  • Raisi: Muqawama umefichua kuwa Israel haina uwezo wa kujihami

Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kambi ya muqawama imeanika njozi na uwezo bandia wa kujihami wa utawala wa Kizayuni wa Israel.

Rais wa Iran amesema hayo hapa mjini Tehran katika mazungumzo yake na Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas), Ismail Haniya na kueleza kuwa, mrengo wa mapambano umefichua kuwa, Israel haina uwezo mkubwa wa kujihami kama inavyojaribu kuwaonyesha walimwengu. 

Sayyid Raisi amebainisha kuwa, ushindi mkubwa wanaoupata Wapalestina katika medani ya vita ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu kutokana na subira yao katika kukabiliana na ukandamizaji na dhulma za utawala wa Kizayuni na waungaji mkono wake.

Rais wa Iran ameongeza kuwa, kukatisha tamaa kizazi cha vijana wa Palestina ili waache kupigania ukombozi wa ardhi zao zinazokaliwa kwa mabavu na utawala ghasibu wa Kizayuni ni moja ya malengo ya Wazayuni katika kujaribu kuanzisha uhusiano wa kawaida na baadhi ya nchi za Kiarabu na Kiislamu.

Rais Raisi amesisitiza kuwa, muqawama upo katika ubora wake hivi sasa na umeleta mlingano wa nguvu si tu Palestina, lakini katika eneo la Asia Magharibi na kimataifa. Ameongeza kuwa, njama za baadhi ya madola kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel hazitafua dafu.

Rais Raisi na Ismail Haniya

Kwa upande wake, Ismail Haniya, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas amesisitiza juu ya umoja katika Palestina inayokaliwa kwa mabavu na kueleza kwamba, taifa la Palestina halina njia nyingine ya kuwatimua wavamizi isipokuwa kuendeleza muqawama, uthabiti na mapigano.

Haniyah amesisitiza kuwa, taifa lililovamiwa na kukaliwa kwa mabavu halitakomboka isipokuwa kwa kuwa na  umoja, na Hamas iko tayari kufanya lolote lile ili kupatikana umoja huo.

Aidha Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina ameipongeza Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa uungaji mkono wake, na kuitaja kama nguzo kuu na muhimu ya mrengo wa muqawama wa Wapalestina. 

Haniya ambaye aliwasili hapa Iran juzi Jumatatu akiongozi ujumbe wa ngazi za juu wa Hamas ameongeza kuwa, si siri kwamba Iran inaipa Harakati hiyo ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina msaada ya kisiasa, kifedha, kijeshi na kiteknolojia.