Kiongozi Muadhamu: Njama za Wazayuni za kuyagawa makundi ya muqawama zimefeli
(last modified Thu, 22 Jun 2023 03:24:12 GMT )
Jun 22, 2023 03:24 UTC
  • Kiongozi Muadhamu: Njama za Wazayuni za kuyagawa makundi ya muqawama zimefeli

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema njama za Wazayuni za kupika majungu ya fitina ili kuibua mifarakano na kuyagawa makundi ya muqawama zimefeli na kusisitiza kwamba, utawala huo wa Kizayuni karibuni utapigishwa magoti na wanamuqawama katika eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Ayatullah Ali Khamenei alisema hayo jana Jumatano hapa mjini Tehran katika mazungumzo yake na Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas), Ismail Haniya na kueleza kuwa, "Nafasi ya kizazi kipya cha vijana wa Kipalestina na kujihusisha kwao na mapambano dhidi ya Wazayuni kuna umuhimu mkubwa na wa kipekee."

Amesema matukio yanayoshuhudiwa hivi sasa katika mji wa Jenin katika eneo la Ukingo wa Magharibi ukiwemo mzingiro uliowekwa na vijana wa Kipalestina dhidi ya vikosi vya Israel, yanaashiria kuwa Wapalestina karibuni hivi watapata ushindi kamili.

Kiongozi Muadhamu amefafanua kwa kusema: Ni nani angelifikiria kwamba siku moja vijana wa Palestina mjini Jenin watavibana vikosi vya Wazayuni kwa kadri kwamba walazimike kutumia ndege za kivita ili kuvunja mzingiro wa wanamuqawama vijana? Lakini hili lilifanyika siku chache zilizopita huko Jenin.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema, "Kadri kadhia ya Palestina inavyozidi kustawi, ndivyo masuala ya umma wa Kiislamu yatazidi kupiga hatua. Ardhi ya Palestina ni milki ya Waislamu wote, na kwa msingi huo Waislamu wote wana jukumu la kuikomboa ardhi hiyo, kwani kufanya hivyo ni kutekeleza wajibu wa kidini."

Kiongozi Muadhamu amesisitiza juu ya umoja katika Palestina inayokaliwa kwa mabavu na kueleza kwamba, taifa la Palestina halina njia nyingine ya kuwatimua wavamizi isipokuwa kuendeleza muqawama. 

Vijana wanamuqawama katika mji wa Jenin

Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa, njama za baadhi ya madola kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel hazitafua dafu. Ameongeza kuwa, licha ya mashinikizo, lakini jamii ya kimataifa imeendelea kusimama na Wapalestina, na hili lilidhihirika zaidi katika Siku ya Quds, ambapo watu walijitokeza kwa wingi hata katika nchi za Ulaya kutangaza upinzani wao dhidi ya Wazayuni.

Kwa upande wake, Ismail Haniya, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas ameipongeza Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa uungaji mkono wake, na kuitaja kama nguzo kuu na muhimu ya mrengo wa muqawama wa Wapalestina. 

Amebainisha kuwa, taifa lililovamiwa na kukaliwa kwa mabavu halitakomboka isipokuwa kwa kuwa na  umoja, na Hamas iko tayari kufanya lolote lile ili kupatikana umoja huo na kuikomboa Quds Tukufu.

Tags