Jul 01, 2023 04:50 UTC
  • Mohammad Baqer Qalibaf
    Mohammad Baqer Qalibaf

Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amesema: Waislamu duniani wanapaswa kufuata misimamo ya viongozi wakuu wa dini na mipaka ya sheria tukufu za Kiislamu, kujibu ipasavyo matusi ya kuchukiza na kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu.

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ameyasema hayo baada ya serikali ya Sweden kuruhusu watu wenye chuki dhidi ya Uislamu kudhalilisha na kuvunjia heshima nakala ya kitabu kitukufu cha Mwenyezi Mungu, Qur'ani nchini humo. Kitendo hicho kiovu kilifanywa na raia wa Sweden katika siku tukufu ya sikukuu ya Idi Jumatano iliyopita.

Akizungumzia ruhusa iliyotolewa na serikali ya Sweden kwa ajili ya kuivunjia heshima Qur'ani Tukufu, Mohammad Baqer Qalibaf, ameongeza kuwa: Hatua ya serikali na polisi ya Sweden ya kudharau na kuidunisha Qur'ani Tukufu kwa kisingizio cha uongo cha uhuru wa kusema na kutenda, inapaswa kulaaniwa vikali.

Spika wa Bunge la Iran amesisitiza kuwa: Waislamu duniani kote watajibu matusi hayo ya kuchukiza kwa mujibu wa misimamo ya viongozi wakuu wa dini na ndani ya fremu ya sheria tukufu za Kiislamu. 

Wakati huo huo wanafunzi wa vyuo vikuu walikusanyika jana mbele ya ubalozi wa Sweden mjini Tehran wakipinga kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu nchini Sweden.

Wanafunzi hao walikuwa wakipiga nara zinazolaani kitendo cha kudhalilisha na kuvunjiwa heshima Qur'ani nchini Sweden na kutoa wito wa kukomeshwa vitendo hivyo viovu.

Jumuiya ya Umma wa Kiislamu (Muslim World League) pia imetoa taarifa kali kulaani kudhalilishwa maandishi matakatifu ya Kiislamu nchini Sweden na kusema kuwa, taswira na picha za kuchomwa moto Qurani Tukufu zinakusudia kuchochea na kuumiza hisia za Waislamu kote duniani, hasa kwa kuzingatia kuwa kitendo hicho kimefanyika katika sikukuu ya Idul Adh'ha.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) pia amelaani jinai hiyo ya kuchomwa moto nakala ya Qurani Tukufu nje ya Msikiti wa Jamia mjini Stockholm nchini Sweden na kuitaka serikali ya Sweden kuwachukulia hatua stahiki wahusika wa hujuma hiyo.

Tags