Rais Raisi: Jumuiya ya Shanghai ina nafasi ya kipekee katika kustawisha mashirikiano
(last modified 2023-07-04T11:46:24+00:00 )
Jul 04, 2023 11:46 UTC
  • Rais Raisi: Jumuiya ya Shanghai ina nafasi ya kipekee katika kustawisha mashirikiano

Rais Ebrahim Raisi amesema Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai ina nafasi ya kipekee katika kustawisha mchakato wa kupanua mashirikiano ya kisiasa, kiusalama na kiuchumi.

Katika kikao cha ishirini na tatu cha Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai kilichofanyika leo kwa njia ya intaneti kwa uwenyeji wa India, uanachama wa kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika jumuiya hiyo umetangazwa, na hati za kujiunga rasmi Iran zimetiwa saini katika mkutano huo na viongozi wa nchi wanachama.

Wakati huohuo Seyed Ebrahim Raisi, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameeleza katika hotuba aliyotoa katika mkutano huo kwamba, nafasi ya Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai katika kustawisha mchakato wa kupanua mashirikiano ya kisiasa, kiusalama na kiuchumi ni ya kipekee na akasema: "ni matumani yangu kuwa kuwemo Iran katika jumuiya hii muhimu na athirifu kutaandaa mazingira kwa ajili ya kudhamini usalama kwa pamoja, kufungua njia kuelekea kwenye ustawi endelevu, kupanua mshikamano na mawasiliano, kuimarisha umoja, kuheshimiwa zaidi haki ya kujitawala ya nchi zote na kushirikiana pamoja katika kukabiliana na matishio ya mazingira".

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema: Ushirikiano wa wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai katika nyanja za nishati, teknolojia, viwanda, kilimo, biashara na masoko unaweza kutoa mwanga mkubwa wa matumaini wa kuwa na nidhamu na utaratibu wa haki wa kikanda mbele ya macho ya mataifa ya dunia.

 

Rais Raisi ametilia mkazo pia umuhimu wa kuondolewa sarafu ya dola katika biashara duniani, na akasema: kwa kutumia mabavu ya kiuchumi na vikwazo, madola ya kibeberu ya Magharibi yamehatarisha usalama na ustawi wa kiuchumi pamoja na misingi ya biashara ya haki na uadilifu duniani.

Katika hotuba yake hiyo, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria pia msimamo wa kuliunga mkono taifa la Palestina na akasema: utawala wa Kizayuni ni nembo halisi ya uchokozi na ukiukaji haki ya mataifa kujitawala. Sambamba na kusisitiza kuwa Iran inaheshimu mamlaka ya kujitawala mataifa yote huru, SEyyed Ebrahim Raisi amesema, Jamhuri ya Kiislamu inalaani pia uingiliaji wowote wa masuala ya ndani ya nchi zingine na inaamini kuwa kuimarisha mamlaka ya kitaifa ndilo suluhisho kuu la kukabiliana na uvurugaji usalama na ugaidi.../

Tags