Feb 12, 2024 04:37 UTC
  • Sheikh Naim Qassim
    Sheikh Naim Qassim

Naibu Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon amesema mrengo wa muqawama haujatangaza vita kamili, lakini iwapo Israel itapanua vita vyake vya Gaza, wanamuqawama hawatasita kufanya mashambulizi ya kujibu chokochoko za adui huyo mpenda vita.

Kanali ya televisheni ya al-Manar imemnukuu Sheikh Naim Qassim akisema hayo na kuongeza kuwa, "Iwapo utawala wa Kizayuni unataka kupanua vita dhidi ya Lebanon, Muqawama wa Kiislamu umejiandaa barabara kukabiliana navyo."

Ameashiria undumakuwili na unafiki wa Marekani juu ya vita vya Gaza na kueleza kuwa, iwapo Washington ingelitaka kusimamisha vita na mashambulizi dhidi ya Wapalestina wa ukanda huo, ingelichukua hatua za kivitendo kwa msingi wa makubaliano yoyote yale, bila kujali iwapo hatua hiyo ingekasirisha utawala haramu wa Israel.

Kadhalika Naibu Katibu Mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon amesema kuwa, Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran lilikuwa tukio kubwa zaidi la karne.

Mauaji ya kimbari yanayofanywa na Israel huko Gaza

Sheikh Naim Qassim amegusia kuhusu msukumo na mafanikio muhimu ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran katika miongo minne na nusu iliyopita, na kuyataja mapinduzi hayo ya 1979 kuwa ndio tukio lenye taathira kubwa zaidi kwa wananchi Waislamu wa eneo la Asia Magharibi.

Aidha Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon ameashiria kusimama kidete Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mbele ya madola dhalimu na ya kibeberu na kutokubali kuburuzwa na kusisitiza kwamba, Iran ni mbeba bendera ya medani ya mapambano na kusimama kidete mkabala wa madhalimu.

Tags