Feb 26, 2024 11:28 UTC
  • Waziri wa Ulinzi wa Yemen: Zama za Marekani na waitifaki wake 'kuhodhi' maji ya kimataifa zimekwisha

Waziri wa Ulinzi wa Yemen amepongeza operesheni za majini zinazoendelea kufanywa na jeshi la nchi hiyo dhidi ya meli zenye uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel katika Bahari Nyekundu kwa lengo la kupinga vita dhidi ya Ghazza, na kusisitiza kwamba zama za "satua ya kuhodhi" Marekani na washirika wake maji ya kimataifa zimekwisha.

Meja Jenerali Mohammed al-Atifi ameyasema hayo katika mahafali ya kuhitimu mafunzo ya kijeshi makadeti wa jeshi Yemen yaliyofanyika katika mji wa Hudaydah ulioko kwenye pwani ya magharibi mwa nchi hiyo.
Jenerali Al-Atifi amesisitiza kwamba, Marekani, Uingereza na Israel lazima zitambue kuwa sera za kuweka mipaka na kudai kuwa na satua ya kuhodhi eneo la maji ya kimataifa zimepitwa na wakati na hazifai tena.
 
Waziri wa Ulinzi wa Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen amebainisha kuwa, Vikosi vya Ulinzi vya Yemen vinaweza kufafanua upya tafsiri ya usalama wa baharini katika Bahari Nyekundu na Bahari ya Arabia kwa uamuzi wake wa kuzuia kupita meli za taifa lolote kuelekea kwenye bandari za maeneo ya Palestina yaliyoanza kukaliwa kwa mabavu na Israel mwaka 1948.
Atifi ameendelea kueleza kwamba, vikosi vya wanamaji vya Yemen vinaweza pia kurejesha utambulisho wa bahari hizo mbili, ambazo zilitekwa nyara na utawala wa Kizayuni.
Makombora ya Vikosi vya Ulinzi vya Yemen

Aidha, Waziri wa Ulinzi wa Yemen ameeleza bayana kuwa, Sana'a inatoa hakikisho kwa mara nyingine tena kwamba Jeshi la Yemen halitalenga meli yoyote, ambayo haina uhusiano na adui wa Kizayuni au kutumikia maslahi yake na kwamba kuna usalama kamili wa safari za vyombo vya majini kwa meli zinazopita Bahari Nyekundu na Bahari ya Arabia.

Atifi amesisitiza pia kwamba, Serikali ya Uokovu wa Kitaifa yenye makao yake makuu mjini Sana’a itaendelea kuheshimu na kutekeleza kikamilifu makubaliano na mikataba yote ya kimataifa, pamoja na mapatano ambayo hayavunji heshima na mamlaka ya kitaifa ya Yemen wala kuweka matakwa na masharti mahususi.

Waziri wa Ulinzi wa Yemen amekumbusha pia kuwa, maadamu mashambulio ya kinyama ya utawala wa Kizayuni yangali yanaendelezwa huko Ghazza, vikosi vya ulinzi vya nchi hiyo vitaendeleza operesheni zake dhidi ya utawala huo ghasibu licha ya Marekani kuulinda na kuusaidia katika kuendeleza vita vyake vya mauaji ya kimbari dhidi ya wananchi madhulumu na wasio na ulinzi wa Palestina.

Wananchi wa Yemen walitangaza uungaji mkono wao wa wazi kwa mapambano ya Palestina dhidi ya utawala wa Kizayuni tangu utawala huo ghasibu ulipoanzisha vita angamizi dhidi ya Ghazza tarehe 7 Oktoba 2023 baada ya harakati za Muqawama wa Palestina kutekeleza operesheni ya kushtukiza na kushangaza ya Kimbunga cha Al-Aqsa.../

Tags