Mar 07, 2024 12:13 UTC
  • Vyombo vya habari vya Uingereza vinawaonyesha Waisraeli waathiriwa zaidi kuliko Wapalestina

Imebainika kuwa "upendeleo mkubwa" unafanywa na vyombo vya habari vya Uingereza katika utangazaji wa matukio ya Ukanda wa Ghaza tangu Oktoba 7, kutokana na kutumia "lugha ya hisia" inayowaonyesha Waisraeli kuwa ni wahanga na waathiriwa wa mashambulizi mara 11 zaidi kulinganisha na Wapalestina.

Hayo ni kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na Kituo cha Ufuatiliaji wa Vyombo vya Habari (CfMM), tawi la Baraza la Waislamu la Uingereza (MCB) chini ya anuani ya "Media Bias Gaza 2023-24", ambayo imefichua kile ilichokitaja kama "upendeleo mkubwa katika utangazaji wa vyombo vya habari" nchini Uingereza kuhusu mzozo wa Israel na Palestina.
 
Utafiti huo wenye maelezo marefu na ya kina umefichua kuwa vituo vingi vya televisheni vya Uingereza vinakuza sana dai la “haki ya Israel kujilinda,” na kufifisha haki za Wapalestina kwa uwiano wa tano kwa moja.
 
Ripoti ya utafiti huo imeendelea kubainisha kuwa, katika matangazo ya televisheni, mitazamo ya Israel inaakisiwa karibu mara tatu zaidi ya ile ya Wapalestina, na katika habari za mtandaoni, ni takribani mara mbili zaidi. Ikifafanua zaidi, ripoti hiyo imesema, kwa upande wa vituo vya televisheni, vimeakisi mitazamo ya utawala wa Kizayuni wa Israel mara 4,311 kulinganisha na ya Wapalestina mara 1,598. Kwa upande wa habari za mitandaoni, vituo vya Uingereza vimeripoti mitazamo ya Israel mara 2,983 kulinganisha na mara 1,737 kuwahusu Wapalestina.

Kwa mujibu wa CfMM, vyombo vya habari vya Uingereza vinatumia "lugha ya hisia" kuwaelezea Waisraeli kama wahasiriwa na waathiriwa wa mashambulio, mara 11 zaidi ya Wapalestina, wakati 76% ya makala za mtandaoni zikionyesha vita vya kinyama vya Israel dhidi ya Wapalestina wa Ghaza kuwa ni vita baina ya Israel na Hamas.

 
Ripoti hiyo ya utafiti imebainisha kuwa, sauti zinazoiunga mkono Palestina zinakabiliwa na upotoshaji na kukosolewa na vyombo vya habari na kwamba habari za mrengo wa kulia na machapisho ya Uingereza ya mrengo wa kulia yamekuwa mstari wa mbele katika kupotosha ukweli kuhusu waandamanaji wanaoiunga mkono Palestina kwa kuwaonyesha kuwa ni watu wenye chuki dhidi ya Mayahudi, wapenda machafuko na wafuasi wa Hamas.
 
Kuhusu matumizi ya lugha, utafiti huo unaonyesha kuwa utangazaji wa vyombo vya habari vya Uingereza umeangazia utumiaji wa lugha ya hisia za kuhuzunisha isiyo na mlingano kwa kuakisi 'mateso' ya Waisraeli huku ikidharau maafa makubwa ya roho za watu wanayoendelea kupata Wapalestina.
 
Ripoti hiyo imeangazia pia uhusiano kati ya Vita vya Ghaza na hisia za chuki dhidi ya Uislamu na kubaini kuwa tangu Oktoba 7 hadi sasa, hisia hizo, hasa uhalifu unaotokana na chuki dhidi ya Uislamu umeongezeka kwa 335%.
 
Faisal Hanif, aliyeongoza timu ya uandishi wa ripoti hiyo amesema, Wapalestina wanastahiki kuripotiwa kama binadamu wenye haki kamili zisizoweza kutenganishwa nao kama wanavyofaidika nazo watu wengine wote.../

Tags