Mar 10, 2024 02:49 UTC
  • Msimamo wa Hamas kuhusu ukwamishaji wa utawala wa Kizayuni katika mazungumzo ya Cairo

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imejiondoka katika mazungumzo ya kusitisha vita mjini Cairo, ikiwa ni jibu lake kwa hatua za ukwamishaji za utawala wa Kizayuni.

Taarifa ya Harakati ya Hamas imeeleza kuwa: "Ujumbe wa Hamas umeondoka Cairo mji mkuu wa Misri kwa ajili ya kufanya mashauriano na viongozi wa harakati hiyo. Hii ni katika hali ambayo mazungumzo ya kusitisha mashambulizii ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Gaza, mchakato wa kuwarejesha wakimbizi na kufikisha misaada ya kibinadamu kwa wakazi wa Ukanda wa Gaza bado yanaendelea. 

Ghazi Hamad mwakilishi wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas pia amesema: Utawala wa Kizayuni hadi sasa haujadhihirisha azma thabiti kwenye mazungumzo kwa ajili ya kufikia mapatano ya kusimamisha vita huko Ukanda wa Gaza na kubadilishana mateka; na usitishaji vita wowote utakaoanzishwa unapasa kuwa kamili na shirikishi na unaokidhi matakwa ya muqawama wa Palestina. 

Ghazi Hamad

Mwakilishi huyo wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas ameongeza kuwa: Tunaendelea na mazungumzo yetu ili kufikia makubaliano ya heshima ambayo yatahakikisha kuwa vita vinasitishwa, wanajeshi ghasibu wanaondoka Ukanda wa Gaza, ujenzi mpya wa Gaza unadhaminiwa na wakimbizi wanarejea katika makazi yao.  

Mazungumzo ya kujadili usitishaji vita Ukanda wa Gaza yalianza huko Cairo Misri tangu tarehe 3 mwezi huu wa Machi kwa kuhudhuriwa na Misri, Marekani, Qatar na ujumbe wa Hamas. Ingawa Hamas na makundi mengine ya muqawama ya Palestina hapo awali yalitangaza masharti yao makuu ya kusimamisha vita; lakini Marekani na utawala wa Kizayuni zinaendelea kukwamisha mazungumzo hayo. Viongozi wa Hamas wameeleza kuwa, kuondoka kikamilifu kwa wanajeshi ghasibu wa utawala wa Kizayuni huko Gaza ndilo sharti lao kuu la kukubali usitishaji vita. Sharti jingine lililotajwa na Hamas pia ni kurejea majumbani mwao wakazi wa Gaza ambao walilazimika kukimbia makazi yao kutokana na mashambulizi ya kikatili ya utawala wa Kizayuni. Suala jingine muhimu ni kuandaliwa mazingira kwa ajili ya ujenzi mpya wa Ukanda wa Gaza ambao umeharibiwa vibaya kufuatia kuendelea vita na mashambulizi ya kikatili ya utawala wa Kizayunidi dhidi ya hospitali, shule, vituo vya elimu na miundombinu ya kiuchumi. 

Ujumbe wa Hamas mjini Cairo

Utawala wa Kizayuni unaendelea kuvuruga mazungumzo ya kusitisha vita licha ya  migogoro ya ndani inayoukabili utawala huo ghasibu kutokana na kuendelea vita dhidi ya Gaza na kuongezeka maandamano ya ndani. Makundi ya mapambano ya Palestina tarehe 7 Oktoba mwaka jana yalianzisha oparesheni kwa jina la Kimbunga cha al Aqsa na kutoa kipigo kwa utawala wa Kizayuni kisichoweza kufidiwa; ambapo serikali ya Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa utawala huo ilikiri wazi kushindwa mbele ya makundi ya mapambano ya Palestina licha ya kuungwa mkono kwa pande zote na Marekani.  

Hii ni katika hali ambayo, katika matukio ya kisiasa ya Gaza; harakati ya Hamas na makundi mengine ya mapambano ya Palestina yako tayari kukubali usitishaji vita iwapo tu misingi ya kuanzisha usitishaji vita itatekelezwa kikamilifu. Rekodi mbaya ya utawala wa Kizayuni ya kupuuza na kutotekeleza mikataba na maazimio ya kimataifa na ya Umoja wa Mataifa inaonesha kuwa, makundi hayo ya muqawama yanatilia mkazo vyema masharti na matakwa yao.

Makundi ya ukombozi ya Palestina yamefikia natija hii kwamba yakabiliane na kusimama imara dhidi ya hatua za kujitanua na vita za utawala wa Kizayuni na kusambaratisha njama na mipango miovu ya Tel Aviv ya kutaka kuitenganisha Gaza na eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan. Aidha kinyume na propaganda za mashirika ya vyombo vya habari vya Marekani na serikali za Magharibi, wananchi na makundi ya mapambano ya Palestina kwa umoja na mshikamano wao yametoa kipigo kisichoweza kufidiwa kwa utawala wa Kizayuni; na muqawama huu umepelekea leo wawakilishi wa Hamas kudhihirisha msimamo madhubuti  katika mazungumzo ya usitishaji vita huko Cairo ili kufanikisha matakwa ya wananchi wa Palestina. 

Matokeo ya  mazungumzo kwa ajili ya kusitisha vita huko Cairo ni kufanikisha matakwa na malengo ambayo yamekuwa yakipambaniwa siku zote; na kukombolewa Quds Tukufu na kuwafukuza maghasibu katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu ni sehemu muhimu na ya msingi ya  malengo hayo. 

Tags