Mar 13, 2024 02:47 UTC
  • Mamia ya walowezi wa Kiyahudi wauvamia Msikiti wa Al-Aqsa huku wakilindwa na askari wa Israel

Mamia ya walowezi wa Kiyahudi jana Jumanne walivamia tena eneo la Msikiti wa Al-Aqsa katika mji wa Baitul-Muqaddas Mashariki unaokaliwa kwa mabavu huku wakisindikizwa na kulindwa na wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel wanaoendelea kuchukua hatua kali za kuwawekea mipaka Wapalestina ya kuingia kwenye msikiti huo.

Kwa mujibu wa shirika rasmi la habari la Palestina Wafa, walowezi hao wa Kizayuni walivamia Msikiti wa Al-Aqsa kwa makundi kutokea eneo la Babul-Mughaaribah upande wa magharibi wa msikiti huo mtakatifu.
 
Mapema siku ya Jumatatu, walowezi wapatao 275 wa Kiyahudi waliingia kwenye eneo la jengo la Msikiti wa Al-Aqsa kwa wito uliotolewa na makundi ya Kiyahudi yenye chuki na itikadi kali wa kushadidisha hujuma na uvamizi katika msikiti huo wakati wa mwezi huu mtukufu wa Ramadhani.
 
Licha ya vizuizi vilivyowekwa na utawala wa Kizayuni vya kuingia ndani ya eneo hilo la tatu kwa utakatifu katika Uislamu, Wapalestina wapatao 35,000 walisali Sala ya Tarawehe siku ya Jumatatu katika Msikiti huo wa Al-Aqsa.

Sala ya Tarawehe ambayo ni Sala ya Sunna husaliwa katika Mfungo wa Ramadhani baada ya Sala ya Isha.

 
Utawala wa Kizayuni wa Israel uliivamia na kuanza kuikalia kwa mabavu Baitul Muqaddas Mashariki, ulipo Msikiti wa Al-Aqsa wakati wa vita vya mwaka 1967 baina yake na Waarabu na hatimaye kuukalia kwa mabavy mji wote wa Quds, mashariki na magharibi yake mwaka 1980 hatua ambayo haitambuliwi kamwe kisheria na Jamii ya Kimataifa.
 
Hali ya wasiwasi imetanda katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan unaokaliwa kwa mabavu tangu utawala haramu wa Israel ulipoanzisha mashambulizi ya kinyama dhidi ya Ukanda wa Ghaza baada ya Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa iliyotekelezwa na Wanamuqawama wa Palestina Oktoba, 7,2023.
 
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Palestina, hadi sasa Wapalestina wapatao 425 wameuawa shahidi na wengine zaidi ya 4,600 wamejeruhiwa katika mashambulio yaliyofanywa na askari wa Kizayuni katika eneo hilo la Ukingo wa Magharibi.../
 

Tags