Apr 23, 2024 07:49 UTC
  • OIC yataka uchunguzi ufanyike kuhusu ‘uhalifu wa kivita’ wa Israel  huko Khan Yunis, Gaza

Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) imetoa wito wa kufanyika uchunguzi kuhusu uhalifu wa kivita wa Israel katika Hospitali ya Nasser huko Gaza ambapo mamia ya miili ya raia imeopolewa kutoka kwenye makaburi ya umati.

Taarifa iliyotolewa Jumatatu na jumuiya hiyo yenye wanachama 57 ililaani mauaji na kuzikwa kwa umati maiti za mamia ya wakazi wa Gaza katika uwanja wa Hospitali ya Nasser kuwa ni "uhalifu wa kivita, uhalifu dhidi ya binadamu na ugaidi wa serikali."

OIC imebainisha waliouawa kuwa ni timu za matabibu, wagonjwa na wakimbizi waliokuwa katika Hospitali ya Nasser.

Shirika hilo limesema kwamba "mamia ya waliokimbia makazi yao, waliojeruhiwa, wagonjwa na timu za matabibu wameteswa na kunyanyaswa kabla ya kunyongwa na kuzikwa kwa umati".

OIC imezitaka Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu na Mahakama ya Kimataifa ya Haki katekeleza majukumu yao kuhusu jinai hii.

Wafanyakazi wa utumishi wa umma huko Gaza wameopoa miili ya Wapalestina 283 katika makaburi kadhaa ya umati katika yadi ya Hospitali ya Nasser, wengi wao wakiwa wanawake, watoto na wazee. Baadhi ya waliouawa walikuwa wamefungwa macho na kufungwa pingu.

Shirika la Afya Duniani lilisema mnamo Aprili 6 kwamba hospitali kubwa zaidi ya eneo la Palestina, al-Shifa, iliharibiwa kabisa mwezi uliopita katika hujuma ya Israel.

Takriban Wapalestina 34,097 wameuawa; wengi wao wakiwa wanawake na watoto, na watu wengine 76,980 wamepata majeraha. Zaidi ya Wapalestina milioni 1.7 wamekuwa wakimbizi wa ndani huko Gaza katika kipindi hiki cha vita.