Jan 05, 2021 07:43 UTC
  • Binti wa shahidi Qassem Suleimani atuma salamu maalum kwa wananchi wa Palestina

Zainab Suleimani, binti wa shahidi Qassem Suleimani ametuma salamu maalum kwa wananchi wa Palestina kwa mnasaba wa maadhimisho maalum yaliyofanyika katika Ukanda wa Gaza kwa anuani ya "Shahidi wa Quds" katika mwaka wa kwanza wa kumbukumbu ya kuuawa shahidi kamanda huyo wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC.

Katika salamu zake hizo, Zainab Suleimani amesema, Shahidi Suleimani amewafunza watoto wake kumtambua adui na kuiashiki Palestina na kibla cha kwanza cha Waislamu kilichoko Quds; na akaongezea kusema: "Quds na Palestina ilikuwa katika kila sehemu ya maisha yetu na wala haikuwa nara na kauli mbiu tu ya kwenye minbari ya hotuba na risasi kwenye mtutu wa jihadi, bali ilikuwa pia mwenendo na mapenzi ya ndani ya familia yetu."

Zainab Suleimani amebainisha kuwa, kwa kuzingatia imani na itikadi yake, baba yake na kabla yake, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Imam Khomeini (MA) wameyaahidi mataifa ya Kiislamu na wanaonyongeshwa hususan mujahidina, kwamba kukombolewa Palestina na ushindi wa walionyongeshwa ni haki na jambo la yakini.

Luteni Jenerali, Shahidi Qassem Suleimani

Katika sehemu nyingine ya ujumbe na salamu zake hizo, binti wa kamanda Qassem Suleimani amewahutubu watu wa Gaza: "Laana ya Mwenyezi Mungu iwashukie watu waliofunga njia za kukufikishieni misaada na wakawa washirika wa jinai za Wazayuni; laana ya Mwenyezi Mungu imshukie kinara wa dhulma duniani, yaani Marekani na madhalimu wote wanaouunga mkono utawala huo mtenda jinai."

Katika hafla hiyo, Mahmoud Az-Zahar, mjumbe wa ofisi ya kisiasa ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema, Luteni Jenerali shahidi Qassem Suleimani hakuwa na ajizi katika kuwaunga mkono wanamapambano wa muqawama kwa msingi kwamba wanamapambano hao wanatetea misingi ya umma; na katika uungaji mkono wa nchi yake hakuwa akitafautisha baina ya wafuasi wa madhehebu tofauti za Kiislamu.

Luteni Jenerali Qassem Suleimani, ambaye usiku wa kuamkia tarehe 3 Januari 2020 alielekea nchini Iraq kwa mwaliko rasmi wa viongozi wa nchi hiyo, aliuliwa shahidi katika shambulio la anga lililofanywa na jeshi vamizi na la kigaidi la Marekani karibu na uwanja wa ndege wa Baghdad alfajiri ya kuamkia siku hiyo.../

Tags