Apr 25, 2021 03:22 UTC
  • Moto waua watu 55 katika hospitali ya wagonjwa wa corona mjini Baghdad, Iraq

Watu wasiopungua 55 wameaga dunia katika ajali ya moto iliyosababishwa na kuripuka mitungi ya oksijini kwenye hospitali moja ya wagonjwa wa corona katika mji mkuu wa Iraq, Baghdad.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Iraq, moto huo umetokea kwenye hospitali ya Ibn Khatib katika eneo la Jisr Diyala, mjini Baghdad. Ripoti zinaeleza kuwa, wagonjwa zaidi ya 55 wa corona wamefariki dunia na wengine wasiopungua 46 wamejeruhiwa kutokana na msongo wa pumzi.

Kwa mujibu wa habari zisizo rasmi, idadi ya vifo inatazamiwa kuongezeka.

Askari wa kikosi cha zimamoto katika operesheni ya kuzima moto huo

Mkurugenzi wa ulinzi wa miji nchini Iraq amesema kuhusiana na ajali hiyo kwamba, wagonjwa 90 na watu wao walio pamoja nao wamenusurika katika ajali hiyo.

Kwa mujibu wa afisa huyo, moto huo umetokea katika ghorofa ya kati ya hospitali hiyo ya Ibn Khatib. Ameongeza kuwa, kutokea kwa moto huo kumepelekea kukatika kwa oksijini wanayopatiwa wagonjwa wa corona na kuifanya hali iwe ngumu zaidi kwa wagonjwa hao.

Waziri Mkuu wa Iraq Mustafa al Kadhimi ametoa amri ya kufanyika uchunguzi wa haraka ili kujua chanzo hasa cha kutokea mkasa huo wa moto katika hospitali hiyo.../

 

Tags