Dec 28, 2021 02:45 UTC
  • Hadi al A'meri
    Hadi al A'meri

Mkuu wa Muungano wa kisiasa wa al Fat-h nchini Iraq amesema, Wairaqi wana deni kubwa kwa Shahidi Qasem Soleimani na Shahidi Abu Mahdi al Muhandis.

Hadi al A'meri amesema hayo sambamba na kutoa mwito kwa wananchi wote wa Iraq kushiriki katika maandamano yatakayofanyika Jumamosi ijayo kwa mnasaba wa kumbukumbu ya kuuawa shahidi Luteni Jenerali Qasem Soleimani, kamanda wa kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) na Abu Mahdi al Muhandis, Naibu Mkuu wa Jeshi la kujitolea la wananchi wa Iraq la al Hashdu Shaa'bi.

Al A'meri amesisitiza kuwa, wananchi wa Iraq wana deni kubwa kwa shahidi Soleimani na shahidi Abu Mahdi al Muhandis, hivyo inapasa wawaenzi na kuwakumbuka mashahidi hao kwa kushiriki kwa wingi katika maadhimisho ya kukumbuka siku waliyouawa shahidi.

Shahidi Qasem Soleimani (kushoto) na shahidi Abu Mahdi al Muhandis

Luteni Jenerali Qasem Suleimani, ambaye mnamo usiku wa kuamkia tarehe 3 Januari 2020 alielekea Iraq kwa mwaliko rasmi wa viongozi wa nchi hiyo, aliuawa shahidi alfajiri ya kuamkia siku hiyo yeye na Abu Mahdi al Muhandis, pamoja na wanamuqawama wengine wanane, katika shambulio la anga lililofanywa na jeshi la kigaidi la Marekani karibu na uwanja wa ndege wa Baghdad.../

Tags