Jun 23, 2022 03:43 UTC
  • Knesset yapiga kura ya kulivunja bunge hilo la utawala wa Kizayuni

Bunge la utawala haramu wa Israel (Knesset) limepiga kura ya kujivunja, na hivyo kuandaa mazingira ya uwezekano wa kurejea madarakani kwa kinara wa chama cha Likud, Benjamin Netanyahu, huku baraza la mawaziri la muungano wa Waziri Mkuu, Naftali Bennett, likiporomoka.

Siku ya Jumatano, Knesset ilichukua hatua hiyo katika usomaji wa awali wa muswada unaotarajiwa kukamilishwa wiki ijayo, ambapo Waziri wa Mambo ya Nje, Yair Lapid atachukua nafasi ya waziri mkuu Bennett kwa muda, chini ya makubaliano yaliyopo.

Hatua hiyo imekuja  siku mbili baada ya Bennett kutangaza mpango wake wa kuvunja baraza la mawaziri wakati wa mkutano wa wanahabari kwenye televisheni.

Tangazo la Jumatatu linakuja baada ya wiki kadhaa za uvumi kwamba muungano tawala - ambao una makundi mengi zaidi katika historia ya utawala bandia wa Israel - ulikuwa ukingoni mwa kuanguka.

Israel sasa inatazamiwa kufanya uchaguzi mkuu wa tano ndani ya miaka minne.

Muungano wa serikali ya Bennet ulipoteza wingi wake mapema mwaka huu na umekabiliwa na uasi kutoka kwa wabunge tofauti katika wiki za hivi majuzi.

Naftali Bennett

Kura za maoni zimetabiri kuwa, chama chenye misimamo mikali cha Likud ambacho kinara wake ni Netanyahu, kitaibuka tena kama chama kikubwa zaidi. Lakini bado haijafahamika iwapo ataweza kupata ungaji mkono unaohitajika kuunda baraza jipya la mawaziri.

Wapinzani wa Netanyahu katika mirengo ya kushoto, kulia na katikati, wameapa kumzuia kurejea madarakani.

Hayo yanajiri siku chache baada Waziri Mkuu wa Israel kuonya juu ya kusambaratika kwa ndani utawala huo wa kibaguzi na kujirudia historia ya kuporomoka utawala wa Kiyahudi.

Tags