Apr 12, 2023 12:48 UTC
  • Netanyahu aamuru Mayahudi wasiingie Msikiti wa Al-Aqsa mpaka mwisho wa Ramadhani

Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel ametangaza kuwa kwa ushauri wa maafisa usalama wa Israel, Mayahudi wasiende katika Msikiti wa Al-Aqsa hadi mwisho wa mwezi wa Ramadhani.

Kwa mujibu wa shirika la habari la ISNA, Wapalestina waliuwekea mashinikizo utawala dhalimu wa Kizayuni baada ya wanajeshi wa Israel kuwavamia waumini waliokuwa kwenye ibada ya itikafu katika Msikiti wa Al-Aqsa, na kumfanya waziri mkuu wa utawala huo haramu Benjamin Netanyahu alazimike kulegeza msimamo katika uamuzi wake kuhusiana na msikiti wa Al-Aqsa na hivyo kuamuru Mayahudi wasiingie kwenye msikiti huo mtakatifu mpaka mwisho wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.
 
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Netanyahu ameviamuru vikosi vya polisi vihakikishe kuwa, kuanzia leo Jumatano hadi mwisho wa Ramadhani, walowezi wa Kiyahudi hawaingii katika eneo la Msikiti wa Al-Aqsa.
Netanyahu

Haya yanajiri licha ya kwamba hapo kabla ilikuwa imetangazwa kuwa walowezi wa Kiyahudi wanaruhusiwa kuuvamia Msikiti wa Al-Aqsa hata katika muda wa siku 10 za mwisho za mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Itamar Ben-Gvir, waziri wa usalama wa ndani wa utawala ghasibu wa Kizayuni ametoa kauli ya kukosoa vikali uamuzi huo wa Netanyahu na kuutaja kuwa ni "kosa kubwa mno".
 
Katika siku za hivi karibuni na kufuatia uvamizi na hujuma za askari wa utawala haramu wa Israel na walowezi wa Kizayuni katika msikiti wa Al-Aqsa na dhidi ya waumini Wapalestina wanaosali msikitini humo, mivutano mikali imezuka kati ya pande hizo mbili, na kupelekea kufanywa mashambulizi ya maroketi kutoka Gaza, Lebanon na Syria dhidi ya maeneo yanayokaliwa kwa mabavu na Israel na vilevile hujuma na mashambulio ya utawala huo wa Kizayuni dhidi ya maeneo yalikofyatuliwa maroketi hayo.../

Tags