Watu kadhaa wakamatwa kwa kula mchana wa Ramadhani Zanzibar
Jeshi la polisi visiwani Zanzibar nchini Tanzania limewatia mbaroni watu 12 kwa tuhuma za kukiuka utaratibu wa dini ya Kiislamu kwa kula mchana hadharani katika kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Abubakar Khamis Ally amesema kufuatia video iliyosambaa mitandaoni ikiwaonyesha baadhi ya watu katika eneo la viwanja vya mnazi mmoja Zanzibar kula hadharani wakati wa mchana wa Ramadhani, jeshi hilo lilifanya msako na kuwakamata watu 12 wakiwa na vielelezo, na kwamba wanaendelea na taratibu nyingine ili kuwafikisha mahakamani.
Aidha ameyataja makosa mengine ni pamoja na unyang’anyi, utumiaji wa mihadarati na makosa mengine, ambapo watuhumiwa wanashikiliwa na polisi na wengine tayari wameshahukumiwa mahakamani.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imetoa onyo kwa wananchi watakaokula hadharani katika kipindi cha mchana wakati wa mwezi huu mtukufu wa Ramadhani na kusisitiza kwamba, hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Utamaduni wa wananchi wa Zanzibar ambayo ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa kuheshimu kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani kwa makundi yote wakiwemo wafuasi wa dini tofauti upo hata kabla ya Mapinduzi ya Januari 12 mwaka 1964.
Wiki iliyopita, polisi wanaosimamia sheria za Kiislamu (Hisbah) katika jimbo la Kano kaskazini mwa Nigeria waliwatia mbaroni makumi ya watu kwa tuhuma za kula mchana hadharani, wakati huu wa funga ya mwezi mtukufu wa Ramadhani. Jimbo la Kano ni moja kati ya majimbo ya Kaskazini mwa Nigeria ambayo yanafuata sheria za Kiislamu tangu mwaka 2000, lakini wanazingatia pia sheria za nchi.