May 30, 2023 02:30 UTC
  • Lobi mpya kuundwa katika bunge la Wazayuni kwa lengo la kuuhodhi msikiti wa Al-Aqsa

Vyombo vya habari vya utawala haramu wa Kizayuni wa Israel vimeripoti habari ya kuundwa "lobi mpya" ya Wazayuni katika Knesset (Bunge) la utawala huo ili kuudhibiti Msikiti wa Al-Aqsa katika mji wa Quds unaokaliwa kwa mabavu.

Wazayuni wamekuwa wakishadidisha hujuma na uvamizi dhidi ya Msikiti wa Al-Aqsa, ili kuandaa mazingira ya kuugawanya msikiti huo kimatumizi kwa maeneo na nyakati maalumu.
Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA gazeti la Kizayuni la Yediot Ahronot limeripoti kuwa baadhi ya wajumbe wa Knesset ya utawala wa Kizayuni wamepanga kuunda lobi itakayopewa jina la "Kwa ajili ya ukombozi wa Mayahudi katika Jabali la Hekalu" linalodaiwa na Wazayuni.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, lengo la kuundwa lobi hiyo ni kuuhodhi na kuudhibiti kikamilifu Msikiti wa Al-Aqsa, na wanachokusudia kufanya Wazayuni hao kupitia bunge lao ni kuchunguza umuhimu wa Msikiti wa Al-Aqsa kwa Wazayuni na hadhi yake mbele ya utawala ghasibu wa Israel.
Msikiti wa Al Aqsa ulipovamiwa na askari makatili wa Israel na unyama waliofanya ndani yake

Wazayuni wamedhamiria kuuhodhi Msikiti wa Al-Aqsa na kisha kuubomoa, kwa sababu kulingana na imani yao hewa na potofu, chini ya msikiti huo kuna hekalu lao na wanataka kujenga hekalu hilo mahala pa Msikiti wa Al-Aqsa, kibla cha kwanza cha Waislamu.

Aidha, Wazayuni wamesema, lengo la kuunda lobi hiyo ni kushamirisha dhana na dai lao kuhusiana na hekalu na uhusiano wake na Mayahudi, na vilevile kushadidisha hujuma na uvamizi dhidi ya Msikiti wa Al-Aqsa na kubainisha umuhimu wa hujuma na uvamizi huo.
Hii si mara ya kwanza kwa Wazayuni kuzungumzia njama na mipango kama hiyo na kuunda lobi kama hizo kwa madhumuni ya kuudhibiti Msikiti wa Al-Aqsa.
Takribani kila siku, walowezi wa Kizayuni wanauvamia Msikiti wa Al-Aqsa, huku watetezi wa msikiti huo nao wakitumia mbinu tofauti kukilinda kibla hicho cha kwanza cha Waislamu.../

Tags