Barua ya malalamiko ya Syria kwa Umoja wa Mataifa
(last modified Fri, 23 Mar 2018 02:21:58 GMT )
Mar 23, 2018 02:21 UTC
  • Barua ya malalamiko ya Syria kwa Umoja wa Mataifa

Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria imeandika barua mbili kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na kwa Rais wa Baraza la Usalama la umoja huo kulalamikia uungaji mkono unaoendelea kufanywa na baadhi ya nchi zenye mfungamano na kambi ya Magharibi kwa makundi ya kigaidi nchini humo.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria imeandika barua hizo kama jibu na radiamali kwa shambulio la kombora lililofanywa na magaidi hivi karibuni kwenye soko moja lililoko kwenye viunga vya mji mkuu wa nchi hiyo Damascus, ambalo liliua na kujeruhi makumi ya watu. Barua hizo zilizoandikwa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria zimebainisha kwamba nchi za kikoloni na mamluki wao katika eneo la Mashariki ya Kati zimeitwisha mzigo wa magaidi nchi na taifa la Syria.

Shambulio la kigaidi lililofanywa nchini Syria

Kwa mujibu wa kituo cha habari cha Syria Online, Ali al-Ahmad, mjumbe wa Akademia ya migogoro ya jiopolitiki cha nchini Syria anasema, uungaji mkono wa Magharibi kwa ugaidi nchini humo ndio sababu ya kushamiri na kuenea baa hilo katika eneo. Jamal Wakim, mhadhiri wa historia na uhusiano wa kimataifa katika vyuo vikuu vya Lebanon, yeye pia ameeleza kwamba ushirikiano wa siri na wa dhahiri ambao umekuwepo kati ya viongozi wa Marekani na wapinzani wa Syria unathibitisha nafasi ambayo Washington imekuwa nayo katika kuanza kwa mgogoro wa nchi hiyo na kuendelea kwake hadi sasa.

Sambamba na kuanza wimbi la Mwamko wa Kiislamu katika eneo la Mashariki ya Kati na Kaskazini ya Afrika, njama za Magharibi ikishirikiana na baadhi ya nchi za Kiarabu ikiwemo Saudi Arabia za kutaka kulidhibiti au kupotosha mkondo wa wimbi hilo katika eneo nazo pia zilishadidi; na Mashariki ya Kati ikaandamwa na dhoruba kubwa ya hujuma na mashambulio ya magaidi wenye uraia wa mataifa mbalimbali yakiwemo ya Magharibi.

Magaidi wa DAESH (ISIS) wa nchini Syria wanaoungwa mkono na Marekani, Saudia na waitifaki wao

Ugaidi huo uliokuwa ukiongozwa na madola ya Magharibi uliwalenga pia wananchi wa Syria; hata hivyo madola hayo yakatumia propaganda za kuhadaa watu ili kuhalalisha yale yaliyokuwa yakifanywa na magaidi nchini humo. Kwa kuenea propaganda hizo, kuanzia mwaka 2011 mgogoro wa Syria ukaanza kwa hujuma na mashambulio ya kila upande yaliyofanywa na makundi ya kigaidi yanayoungwa mkono na Saudi Arabia, Marekani na waitifaki wao kwa lengo la kuipindua serikali halali ya Syria inayoongozwa na Rais Bashar al-Assad.

Ripoti mbalimbali zilizofichua ukweli halisi wa mgogoro wa Syria zimezidi kuwafumbua macho walimwengu na kuelewa uhakika kwamba mgogoro wa nchi hiyo ya Kiarabu ni matokeo ya uingiliaji na uwashaji moto wa fitna uliofanywa na madola ya Magharibi na baadhi ya tawala za nchi za Kiarabu. Tukiutupia jicho mgogoro wa Syria tutabaini kuwa kwa kutumia kisingizio cha baadhi ya masuala yaliyokuwa yakilalamikiwa na wananchi ya kutaka mageuzi nchini humo, nchi za Magharibi na baadhi ya nchi za Kiarabu ziliingilia masuala ya ndani ya taifa hilo la Kiarabu kwa kutuma huko maelfu ya magaidi na kuzipa sura ya malalamiko ya wananchi jinai ambazo zimekuwa zikifanywa na magaidi hao.

Rais Bashar al-Assad wa Syria akihutubia wananchi

Uingiliaji haribifu wa maajinabi wanaoongozwa na Marekani ikishirikiana na Saudia na baadhi ya nchi nyingine za eneo huko nchini Syria uligeuza mkondo wa matukio ya nchi hiyo wa kuleta mageuzi ya kisiasa kupitia mazungumzo ya maelewano kati ya wananchi na serikali yao kwa kuifanya Syria shimo la moto wa vita angamizi vilivyoteketeza roho za mamia ya maelfu ya watu, miundombinu ya nchi hiyo na kuwafanya wakimbizi mamilioni ya raia. Njama dhidi ya Syria inapasa zitathminiwe katika fremu ya uingiliaji wa maajinabi  wa Magharibi na mamluki wao katika eneo hili la Mashariki ya Kati yaani watawala wa baadhi ya nchi za Kiarabu kwa lengo la kuzigawa na kuzidhoofisha nchi za eneo hili; kitendo ambacho kimetolewa indhari na kulalamikiwa vikali na Syria.

Katika mazingira kama hayo, viongozi wa serikali ya Damascus wameuandikia barua Umoja wa Mataifa kubainisha malalamiko yao kutokana na kimya kinachoendelea kuonyeshwa na umoja huo mbele ya njama mbalimbali zinazofanywa na madola ya kibeberu ya Magharibi dhidi ya nchi za Mashariki ya Kati.../

Tags