Asilimia 2 ya wahajiri wote duniani wanaishi Iran
Nchini Iran kuna wahajiri milioni nne ambao ni asilimia mbili ya wahajiri wote duniani katika hali ambayo idadi ya watu wa Iran ni asilimia moja ya watu wote wa dunia.
Bahman Eshqi, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tehran ameyasema hayo katika kongamano la kujadili uwezo wa kiuchumi na kibiashara wa wahajiri katika kustawisha uhusiano na nchi jirani.
Ameashiria mtazamo wa kibinadamu na kijamii kwa kadhia ya wahajiri na kusema kuwa, kila ongezeko la asilimia 10 la wahajiri hupelekea kuwepo ongezeko la asilimia 1.5 la kiwango cha biashara na kuongeza kuwa: "Kiwango kikubwa cha bidhaa za Iran zinazouzwa nje ya nchi hupelekwa nchi jirani za Iraq na Afghanistan kupitia wahajiri wa nchi hizo walioko Iran."
Vilevile amesema Iran iko katika eneo la kijiografia lenye taharuki nyingi katika kipindi cha karne kadhaa na hali hiyo inaendelea.
Eshqi amesema kuwa, ukuruba wa kidini na kiutamaduni ni jambo linalowafanya wahajiri wa Iraq na Afghanistan wafadhilishe kuishi Iran baada ya nchi zao kukumbwa na misukosuko. Amesema nukta hizo za pamoja zinapaswa kutumiwa vizuri na kuwa fursa.