Marekani yaziwekea vikwazo benki 14 za Iraq kwa kushirikiana na Iran
Marekani imetangaza kuziwekea vikwazo benki 14 za Iraq kwa tuhuma za kushirikiana na Iran.
Kwa mujibu wa gazeti la Wall Street Journal, Wizara ya Hazina ya Marekani na Benki Kuu ya nchi hiyo mjini New York zinaituhumu Iraq kuwa inafanya miamala kwa kutumia sarafu ya dola ya Marekani na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Gazeti hilo limenukuu maafisa wa Washington wakisema kuwa, Wizara ya Hazina ya Marekani imezizuia na kuziwekea vizingiti benki hizo za Iraq kufanya miamala yoyote kwa kutumia sarafu ya dola.
Marekani inahesabiwa kuwa nchi inayoongoza kwa uwekaji vikwazo duniani, ikiwa na rekodi kubwa zaidi ya kutumia kila aina ya vikwazo dhidi ya nchi zingine kwa ajili ya kufanikisha malengo na maslahi yake.
Machi mwaka huu pia, Marekani ilitangaza kuyawekea vikwazo makumi ya mashirika kwa tuhuma za kuisaidia Iran kukwepa vizingiti vya Washington vya kuiweka Tehran nje ya mfumo wa kimataifa wa fedha.
Kabla ya hapo, Marekani iliyawekea vikwazo makampuni na meli kadhaa katika kuendeleza muelekeo wake wa kiundumakuwili na sera yake ya mashinikizo ya juu kabisa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Marekani imekuwa ikiendeleza na uraibu wake huo wa vikwazo kwa kuyawekea vikwazo mashirika na nchi ambazo hazikubaliani na sera zake za kibeberu.