Gavana wa Karbala: Mazuwari wa Arubaini mwaka huu kupindukia milioni 30
Gavana wa jiji la Karbala nchini Iraq amesema mji huo mtakatifu utapokea wafanyaziara zaidi ya milioni 30 katika Arubaini ya Imam Hussein AS mwaka huu.
Nasif al-Khatabi amesema zaidi ya Mazuwari milioni 14 walikuwa wamewasili katika mji huo mtakatifu kufikia Jumamosi iliyopita.
Gavana huyo ameeleza bayana kuwa, mjumuiko wa Arubaini ya mwaka huu utakuwa mkubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa katika miaka ya hivi karibu.
Al-Khatabi amesema, "Idadi ya wafanyaziara wa Arubaini ya mwaka huu itaongezeka kwa asilimia 50, kutoka milioni 21 mwaka jana hadi milioni 30 mwaka huu."
Mjumuiko wa Arubaini huko Karbala Iraq, unatajwa kuwa mjumuiko mkubwa zaidi wa kidini ulimwenguni, unaowaleta pamoja mamilioni ya wafanyaziara kutoka Iraq na Iran na pia mataifa mengine duniani.
Tukio hilo la kila mwaka, ambalo ni moja ya mikusanyiko mikubwa ya kidini duniani, huleta pamoja umati wa wapenzi na waumini wa Imam Hussein AS kutoka mataifa mbalimbali wanaofanya matembezi ya kilomita 80 kati ya miji mitakatifu ya Najaf na Karbala.
Kwa muda wa wiki kadhaa zilizopita, wafanyaziara kutoka nchi kadhaa zikiwemo Iran, Afghanistan, Pakistan, Jamhuri Azerbaijan, Bahrain, Kuwait na Saudi Arabia wamekuwa wakiwasili Karbala, iliyoko takriban kilomita 100 kusini magharibi mwa mji mkuu wa Iraq, Baghdad.
Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Iran amesema kwamba wafanyaziara wa Iran zaidi ya milioni tatu na laki nane wamemiminika Iraq kushiriki katika kumbukumbu za Arubaini ya Imam Hussein AS mwaka huu, na kwamba zaidi ya milioni mbili na laki tatu tayari wamekwisharejea nchini.