Hizbullah yaikosoa Bahrain kwa kuruhusu kufunguliwa ubalozi wa Israel
Harakati ya Muqawama ya Hizbullah ya Lebanon imeujia juu utawala wa Aal-Khalifa wa Bahrain kwa kuuruhusu utawala haramu wa Israel kufungua ubalozi wake katika nchi hiyo ya Kiarabu ya Ghuba ya Uajemi.
Katika taarifa, Hizbullah imesema utawala wa Manama upo katika mkondo wa kuporomoka kisiasa na kimaadili, kwa kushinikiza uhusiano wa kawaida na adui Mzayuni, baada ya miaka mingi ya kulikandamiza taifa la Bahrain.
Harakati hiyo ya mapambano ya Kiislamu ya Lebanon imeeleza kuwa, hatua ya Aal-Khalifa kuipa ridhaa Israel ya kufungua ubalozi wake nchini Bahrain ni pigo kwa taifa la Palestina ambalo hivi sasa lipo katika mapambano na operesheni za kishujaa mkabala wa ugaidi pofu wa Wazayuni.
Hizbullah imetoa mwito kwa taifa la Bahrain na mataifa mengine ya Waislamu kuendelea kusimama kidete kupinga uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni, ikisisitiza kuwa Israel haifai kuwa na kimbilio salama popote katika eneo.
Mapema mwaka huu, wanazuoni wa Bahrain walikosoa vikali pia mpango wa Aal-Khalifa wa kuwauzia ardhi Wazayuni wakisisitiza kuwa, kitendo hicho ni sawa na kuiuza nchi na ni haramu.
Septemba 2020, viongozi wa Bahrain na wa utawala haramu wa Israel walisaini makubaliano ya kuanzisha uhusiano wa kawaida katika hafla iliyofanyika Ikulu ya White House mbele ya rais wa wakati huo wa Marekani, Donald Trump.
Kufuatia kusainiwa makubaliano hayo ya kuanzishwa uhusiano wa kawaida kati ya Bahrain na utawala haramu wa Israel, wananchi wa Bahrain mara kwa mara wamekuwa wakifanya maandamano ya kupinga uhusiano huo.