HAMAS: Katu hatutauacha peke yake msikiti wa al-Aqswa
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imetangaza kuwa, katu harakati hiyo haitauacha mkono msikiti mtakatifu wa al-Aqswa, kibla cha kwanza cha Waislamu.
Hayo yamesemwa na Muhammad Hamada, msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS huko Quds inayokaliwa kwa mabavu ambaye amesisitiza pia kwamba, Wapalestina hawatasalimu amri mbele ya hujuma na uvamizi wa kila mara wa walowezi wa Kizayuni dhidi ya eneo hilo takatifu.
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) imekuwa ikisisitiza mara kwa mara kuwa, msikiti wa al-Aqswa utaendelea kubakia kuwa mstari mwekundu wa Waislamu na kwamba, kila mkono wenye lengo la kuuvunjia heshima msikiti huo utakatwa.
Msikiti wa al-Aqswa unajulikana kuwa nembo kuu ya utambulisho wa Kiislamu na Kipalestina wa eneo takatifu la Quds na utawala wa Israel unajaribu kuharibu utambulisho huo, lakini kusimama imara na kuwa macho wananchi wa Palestina kumeufedhehesha utawala huo wa Kizayuni na kupelekea njama zake kushindwa.
Israel inashadidisha vitendo vyake haramu na kubadili muundo wa kijiografia na kijamii wa mji wa Quds sambamba na kufuta utambulisho na utamaduni wa Kiarabu kupitia mipango yake ya ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni na miundomsingi inayohusiana na vitongoji hivyo ikiwemo na kujenga barabara na njia ya chini kwa chini.
Hujuma za walowezi wa Kizayuni dhidi ya msikiti wa al-Aqswa vimekithiri zaidi baada ya kuingia madarakani serikali yenye misimamo mikali ya Benjamin Netanyahu ambayo imekuwa ikionyesha chuki za wazi wazi dhidi ya Wapalestina na maeneo yao matakatifu.
Vitendo vya kuyavunjia heshima matukufu ya Kiislamu huko Palestina vinafanyika katika hali ambayo, viongozi wa nchi za Kiarabu na jamii ya kimataifa wameendelea kunyamaza kimya na kutochukua hatua zozote za maana za kukabiliana na vitendo hivyo vinavyokinzana na utu na ubinadamu.