Ansarullah: Kimbunga cha al-Aqsa ni ushindi wa kihistoria
Katibu Mkuu wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen amepongeza Operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa na kueleza kuwa, shambulizi la kushtukiza la Harakati ya Muqawama wa Kiislamu wa Palestina (HAMAS) na makundi mengine ya mapambano ya Palestina dhidi ya Israel ni ushindi wa kihistoria ambao umeleta mlingano wa nguvu na kuusabababishia hasara kubwa utawala wa Kizayuni wa Israel.
Abdul Malik al Houthi aliyasema hayo jana Jumanne katika hotuba iliyorushwa kupitia televisheni mjini Sana'a na kuongeza kuwa, "Operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa ni jibu halali dhidi ya uvamizi na jinai za Wazayuni kwa Wapalestina kwa miongo kadhaa."
Amebainisha kuwa: Kimbunga cha al-Aqsa ni operesheni kubwa, yenye umuhimu na ambayo imefanyika sambamba na haki halali ya wapambanaji wa Palestina na taifa la Palestina kwa ujumla, kukabiliana na maadui zao na kuzima dhulma na jinai za utawala huo pandikizi.
Al Houthi amesema utawala huo haramu unaua wanawake na watoto wa Kipalestina kila uchao, na kuwanyima haki zao kama vilke haki ya uhuru na mamlaka ya kujitawala, mbali na kulalia kwa mabavu ardhi zao.
Kiongozi huyo amekosoa vikali hujuma na jinai za utawala wa Kizayuuni wa Israel dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina na kutaka kudumishwa uungaji mkono kwa wananchi hao madhulumu.
Hali kadhalika kiongozi huyo wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen ameutaka utawala wa Kizayuni wa Israel uachane na hatua zake za kinyama dhidi ya Baytul-Muqaddas na Masjidul Aqsa.
Aidha Marekani ni mshirika wa utawala wa Kizayuni wa Israel katika vitendo vyake vya jinai dhidi ya watoto, wanawake na raia wasio na hatia wa Palestina. Amesema nchi zinazoipa Israel kila aina ya misaada zikiongozwa na Marekani, zinabeba dhima ya jinai za kutisha zinazofanywa na Tel Aviv dhidi ya Wapalestina madhulumu.