Aug 09, 2024 07:19 UTC
  • Al-Houthi: Juhudi za Magharibi hazitazuia jibu la Iran kwa Israel

Kiongozi wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen amesisitiza kuwa, kucheleweshwa kwa jibu la mhimili wa Muqawama na Iran dhidi ya jinai na ukatili wa utawala wa Kizayuni ni suala la kimkakati ili kutoa nafasi ya kuligeuza kuwa jibu madhubuti.

Kwa mujibu wa mtandao wa habari wa Al Masirah wa Yemen , Abdul-Malik al-Houthi alisema siku ya Alhamisi kuwa, mauaji ya kiongozi wa kisiasa wa HAMAS, Ismail Haniyah na kamanda mkuu wa Hizbullah, Fuad Shukr yameathiri na kuligusa eneo zima.

"Adui Mzayuni yuko katika hali ya taharuki na hofu kubwa baada ya kuzusha mivutano ya hatari," kiongozi wa Ansarullah amesema na kuongeza kuwa, "Mmaafisa wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wamesisitiza kuwa, jibu la jinai za utawala wa Kizayuni ni jambo lisiloepukika, na kilichotokea hakiwezi kupuuzwa kwa namna yoyote ile."

Kiongozi wa Ansarullah amesisitiza kuwa, vita dhidi ya Israel hivi sasa viko katika kilele chake baada ya mauaji yaliyofanywa na utawala huo pandikizi dhidi ya Kiongozi wa Kisiasa wa HAMAS, Ismail Haniyeh na kamanda wa Harakati ya Muqawama ya Hizbullah ya Lebanon, Fuad Shukr.

Ameeleza bayana kuwa, wakuu wa kambi ya Muqawama wamethibitisha kwamba, jinai zinazofanywa na maadui haziwatetereshi hata kidogo, bali zinaongeza tu ari na moyo wao wa Jihadi na Muqawama. Abdul Malik al Houthi amesema kuwa, kuuawa shahidi katika njia ya haki ni sehemu ya maisha ya viongozi na makamanda wa Muqawama na kwamba, kwa jinai zake hizo, utawala wa Kizayuni wa Israel umejisogeza karibu zaidi na maangamizi yake kama inavyosema ahadi ya Allah.

Kadhalika Al-Houthi ameendelea kusema kuwa, hakuna chembe ya shaka kuwa Yemen itatoa jibu kwa hujuma za mwezi uliopita za utawala wa Israel dhidi ya mji wa bandari wa Hudeidah.

Tags