Israel yashambulia kwa makombora viwanja vya ndege Syria
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i103420-israel_yashambulia_kwa_makombora_viwanja_vya_ndege_syria
Vikosi vya jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel vimefanya mashambulizi ya anga kwa kutumia makombora dhidi ya viwanja viwili vya ndege nchini Syria; wakati huu ambapo dunia inaendelea kulaani mashambulizi ya anga ya utawala wa Tel Aviv katika maeneo ya makazi ya raia huko katika Ukanda wa Gaza ili kujaribu kufidia kipigo ulichopata kutoka kwa wapambanaji wa Hamas.
(last modified 2026-03-17T04:36:21+00:00 )
Oct 13, 2023 03:43 UTC
  • Israel yashambulia kwa makombora viwanja vya ndege Syria

Vikosi vya jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel vimefanya mashambulizi ya anga kwa kutumia makombora dhidi ya viwanja viwili vya ndege nchini Syria; wakati huu ambapo dunia inaendelea kulaani mashambulizi ya anga ya utawala wa Tel Aviv katika maeneo ya makazi ya raia huko katika Ukanda wa Gaza ili kujaribu kufidia kipigo ulichopata kutoka kwa wapambanaji wa Hamas.

Shirika rasmi la habari la Syria SANA limenukuu duru za kijeshi nchini humo zikieleza kuwa, wanajeshi wa Israel jana Alkhamisi walishambulia kwa makombora uwanja wa ndege katika mji mkuu Damascus na uwanja mwingine mjini Halab (Aleppo), kaskazini mwa nchi.

Duru za kiusalama zimeripoti kuwa, Wazayuni walishambulia viwanja hivyo vya ndege kwa wakati mmoja na kuharibu barabara za kutua ndege kwenye viwanja hivyo, na hivyo angatua hizo zimelazimika kusitisha huduma zao.

Askari mmoja wa jeshi la Syria ambaye hakutaka jina lake litajwe ameiambia SANA kuwa, hujuma hizo dhidi ya viwanja vya ndege vya nchi hiyo ya Kiarabu zikakusudia kupotosha fikra za waliowengi duniani, ili wasishughulishwe na mashambulizi ya kinyama ya Israel dhidi ya watu wa Gaza.

Hili ni shambulizi la kwanza la Wazayuni dhidi ya Syria tangu kuanza kwa Operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa katika ardhi za Wapalestina zinazokaliwa kwa mabavu; ingawaje utawala huo pandikizi umekuwa ukishambulia maeneo mbalimbali ya Syria kwa miaka mingi sasa.

Wajuzi wa mambo wamekosoa mienendo hiyo ya Israel ya kufanya mashambulizi yake ya makombora bila kujali ndege za abiria zinazoruka katika anga ya Syria wakisisitiza kuwa, kitendo hicho kinaonyesha namna Tel Aviv isivyoyapa thamani maisha ya wanadamu hususan raia ya kawaida.