Abdollahian: Wamagharibi wanapotosha ukweli ili wahalalishe jinai za israel huko Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i103462-abdollahian_wamagharibi_wanapotosha_ukweli_ili_wahalalishe_jinai_za_israel_huko_gaza
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema nchi za Magharibi zinafuatilia kupotosha ukweli wa mambo juu ya matukio yanayoshuhudiwa katika Ukanda wa Gaza, ili kwa njia hiyo zihalalishe jinai zinazofanywa na utawala haramu wa Israel dhidi ya Wapalestina wanaoishi katika eneo hilo la Palestina linalokaliwa kwa mabavu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 14, 2023 04:20 UTC
  • Abdollahian: Wamagharibi wanapotosha ukweli ili wahalalishe jinai za israel huko Gaza

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema nchi za Magharibi zinafuatilia kupotosha ukweli wa mambo juu ya matukio yanayoshuhudiwa katika Ukanda wa Gaza, ili kwa njia hiyo zihalalishe jinai zinazofanywa na utawala haramu wa Israel dhidi ya Wapalestina wanaoishi katika eneo hilo la Palestina linalokaliwa kwa mabavu.

Kwa mujibu wa kanali ya Press TV, Hossein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amesema hayo katika mazungumzo yake na Rais Bashar al-Assad wa Syria mjini Damascus jana jioni na kueleza kuwa, kambi ya muqawama ina uwezo kusimama kidete dhidi ya utawala wa kibaguzi wa Israel kwa muda mrefu.

Kadhalika amekosoa mwito wa Washington wa kuyataka makundi ya Palestina eti kujizuia, na wakati huohuo, inaupa utawala wa Kizayuni kila aina ya silaha zinazotumika dhidi ya wananchi wasio na hatia katika Ukanda wa Gaza.

Amir-Abdollahian ameyataja mauaji ya watoto, wanawake na wakongwe katika Ukanda wa Gaza kama jinai za kivita, ambapo pia amekosoa mzingiro wa kila upande dhidi ya wakazi wa Gaza.

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema sera za kuchupa mipaka za Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel, Benjamin Netanyahu ndiyo sababu kuu ya kuanzishwa Operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa.

Hujuma za anga za Israel Ukanda wa Gaza

Kwa upande wake, Rais Bashar al-Assad wa Syria ameeleza wasiwasi wake juu ya ukubwa wa jinai za utawala pandikizi wa Israel dhidi ya wakazi wa Gaza na kusema kuwa, mamlaka za Tel Aviv zinataka kutumia mashambulizi ya Palestina kama kisababu cha kuuangamiza mrengo wa muqawama.

Zaidi ya Wapalestina 1,900 wameuawa shahidi katika mashambulizi ya anga ya utawala haramu wa Israel dhidi ya eneo la Ukanda wa Gaza, wakiwemo watoto 614 na wanawake 370. Aidha Wapalestina 7,696 wamejeruhiwa.