Sababu na matokeo ya kuuzuliwa Spika wa Bunge la Iraq
(last modified Sat, 18 Nov 2023 06:44:44 GMT )
Nov 18, 2023 06:44 UTC
  • Sababu na matokeo ya kuuzuliwa Spika wa Bunge la Iraq

Jumanne iliyopita, Mahakama ya Juu ya Iraq ilimuuzulu Spika wa Bunge la nchi hiyo, Mohammad Al-Halbousi.

Mnamo mwaka 2022, Mohammad Al-Halbousi alichaguliwa kwa mara ya pili kuwa Spika wa Bunge la Iraq. Takribani miaka miwili imepita katika muhula wa pili wa Uspika na jumla ya miaka sita tangu Mohammad Al-Halbousi aliposhika wadhifa wa Spika wa Bunge la Iraq, mpaka Mahakama ya Juu ya nchi hiyo ilipotoa hukumu siku ya Jumanne ya kuamuru auzuliwe.
 
Zimetajwa sababu kadhaa zilizopelekea kuuzuliwa Al-Halbousi, lakini mtazamo wenye nguvu ni kwamba Spika huyo alikiuka sheria iliyopitishwa na Bunge la Iraq ya kujinaisha kuanzisha ushirikiano wa aina yoyote na utawala wa Kizayuni wa Israel na makampuni yenye uraia wa utawala huo ghasibu. Kwa mujibu wa sheria ya "uhalifu wa kuanzisha uhusiano", mwanasiasa yeyote wa Iraq hana haki ya kusaini mikataba ya kibiashara na makampuni ya kimataifa ambayo miongoni mwa wenye hisa katika makampuni hayo ni Wazayuni. Aidha, hakuna chama au afisa yeyote wa Iraq mwenye haki ya kutia saini mikataba na makampuni ambayo kazi yake moja ni kufanikisha kuanzishwa uhusiano kati ya nchi mbalimbali na utawala wa Kizayuni.
Ehud Barak

Basem Derakhshan, mbunge binafsi katika Bunge la Iraq ambaye alifungua mashtaka dhidi ya Mohammad al-Halbousi, aliwasilisha mahakamani nyaraka zinazoonyesha ukiukaji wa sheria uliofanywa na spika huyo aliyeondolewa madarakani. Akiwa Kiongozi wa Chama cha Taqaddum, Mohammad Al-Halbousi alitia saini mkataba na kampuni ya kigeni ambayo ilihusika katika kufanikisha mpango wa kuanzishwa uhusiano kati ya utawala wa Kizayuni na nchi kadhaa. Mshauri mkuu wa kampuni hiyo ni Ehud Barak, waziri mkuu wa zamani wa utawala haramu wa Kizayuni. Kwa hakika sababu kuu iliyopelekea mahakama ya Iraq kumuuzulu al-Halbousi ilikuwa ni hiyo ya kukiuka sheria ya kujinaisha kuanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel. Uamuzi huo wa Bunge la Iraq, ambao umechukuliwa wakati utawala katili wa Kizayuni unaendelea kufanya mauaji ya kimbari na ya halaiki huko Gaza kwa zaidi ya siku 40 sasa, unaweza ukawa ni hatua mojawapo ya kuiunga mkono kivitendo Palestina.

 
Sababu nyingine ya kuuzuliwa Mohammad al-Halbousi inahusiana na utumiaji mbaya wa madaraka. Inasemekana kuwa, kutokana na tofauti zilizokuwepo baina yake na mbunge Leith Al-Dulaimi, Spika huyo alighushi barua ya kujiuzulu mbunge huyo na kumfanya Al-Dulaimi afungue kesi dhidi yake katika Mahakama ya Juu ya Iraq. Al-Dulaimi alikuwa mwanachama wa chama cha Taqddum kinachoongozwa na Al-Halbousi, lakini aliamua kukihama chama hicho. Hata hivyo, Mohammad Al-Halbousi, ambaye alikuwa na mivutano na al-Dulaimi ndani ya Chama cha Taqaddum, alifanya hila ya kutaka kuonyesha kuwa kujiuzulu kwa mbunge huyo hakukuhusiana na kujitoa kwenye Mrengo wa Chama cha Taqddum tu bungeni, bali pia ni kujiuzulu wadhifa wake wa Ubunge. Kwa hiyo, kwa nafasi yake ya Uspika, Al-Halbousi alitangaza rasmi kukubali kujiuzulu kwa Leith Al-Dulaimi na kuanzisha mchakato wa kutafuta mbunge wa kujaza nafasi yake. Hata hivyo, Leith Al-Dulaimi alitangaza kuwa hajachukua katu uamuzi wa kujiuzulu ubunge na kwamba barua ya kujiuzulu iliyohusishwa na yeye ilighushiwa na Al-Halbousi. Kwa sababu hiyo alifungua keshi dhidi ya spika huyo katika Mahakama ya Juu ya Katiba.
Mohammad al-Halbousi

Mohammad Al-Halbousi alikuwa Spika wa Bunge la Iraq akiwakilisha jamii ya Masuni wa nchi hiyo. Kutokana na kuuzuliwa wadhifa huo, Mohsen al-Mandlawi, naibu wa kwanza wa Spika kutoka jamii ya Mashia, ndiye anayekaimu nafasi hiyo kwa sasa hadi Spika mpya atakapochaguliwa. Kwa kuzingatia kuwa Al-Mandlawi ni Mshia, hatoweza kukalia kiti cha Uspika kwa muda mrefu.

 
Suala jengine muhimu ni kwamba baada ya kutolewa hukumu wa kuuzuliwa Al-Halbousi, viongozi na wabunge wa Chama cha Taqaddum walifanya kikao na kupitisha uamuzi wa kususia vikao vya Baraza la Mawaziri. Aidha, viongozi hao wa Chama cha Taqaddum walipitisha uamuzi wa kuwataka wawakilishi wao watatu waliomo katika Serikali ya Shirikisho wajiuzulu pia. Kwa mujibu wa uamuzi uliochukuliwa na  Chama cha Taqaddum, wabunge wa chama hicho nao pia watasusia vikao vyote vya Bunge la nchi hiyo. Inavyoonekana, kujiuzulu wawakilishi na wabunge wa chama hicho serikalini na bungeni kunaweza kupelekea kuibuka duru mpya ya changamoto za kisiasa nchini Iraq.../

 

Tags