Mashirika ya haki Palestina yaonya kuhusu 'Nakba ya Pili' Gaza
(last modified Tue, 05 Dec 2023 06:52:53 GMT )
Dec 05, 2023 06:52 UTC
  • Mashirika ya haki Palestina yaonya kuhusu 'Nakba ya Pili' Gaza

Mashirika matatu ya kutetea haki za binadamu ya Palestina yameashiria hatua ya Israel ya kuwafukuza kwa umati Wapalestina katika Ukanda wa Gaza na kutahadharisha kuwa, utawala huo wa Kizayuni unapanga kukariri Nakba ya pili katika eneo hilo lililozingirwa.

Indhari hiyo imetolewa na mashariki ya Palestinian Center for Human Rights (Kituo cha Haki za Binadamu cha Palestina), Al Mezan Center (kituo cha Al Mezan), na Al-Haq Foundation for Human Rights (Wakfu wa Haki za Binadamu wa Al-Haq) ambayo yameonya kuwa, Israel inapanga kukariri tukio kuwafurusha Wapalestina katika makazi yao ya asili kama ilivyofanya mwaka 1948.

Ikumbukwe kuwa, tarehe 15 Mei 1948, ambayo inajulikana kwa jina la "Nakba" katika historia ya Palestina, ni siku ambayo Wazayuni walivamia, kuua na kuwafukuza Wapalestina zaidi ya 750,000 katika miji yao na kuharibu takriban vijiji 530.

Mashirika hayo matatu ya kutetea haki za binadamu ya Palestina yameeleza katika taarifa kuwa: Israel inang'ang'ania mpango wake wa kuwafukuza wakazi wa Ukanda wa Gaza nje ya mipaka yao tangu ianzishe vita dhidi ya ukanda huo mnamo Oktoba 7. 

UNRWA: Vita vya Israel vimefanya watu milioni 1.9 kuhama makazi yao Gaza tangu Oktoba 7

Mamlaka za utawala ghasibu wa Israel zimetoa mara kwa mara mwito wa kuhamishwa kwa wingi kwa wakimbizi wa Gaza na kupelekwa katika jangwa la Sinai nchini Misri au kupelekwa katika nchi za Kiarabu kama Jordan na hata Ulaya.

Aidha mwezi uliopita, maafisa wa Umoja wa Mataifa sambamba na kutahadharisha kuwa, utawala wa Kizayuni unapanga kukariri Nakba ya Pili huko Gaza walitangaza kuwa, Israel inatumia mbinu ya kukata mawasiliano ya simu na intaneti ili kuficha jinai zake.

Mashariki ya haki za binadamu ya Palestinian Center for Human Rights, Al Mezan Center, na Al-Haq Foundation for Human Rights yanasisitiza kuwa, hatua ya Wazayuni ya kuwafurusha kwa nguvu mamia ya maelfu ya Wapalestina na kuwaelekeza Rafah na kisha katika mipaka ya Misri imeibua wasiwasi wa kuibuka 'Nakba ya Pili' dhidi ya Wapalestina.