Iraq yazitahadharisha nchi zinazowafadhili magaidi
Waziri Mkuu wa Iraq ametoa radiamali yake kwa mashambulizi ya kigaidi yaliyoutikisa mji mkuu wa nchi hiyo Baghdad hivi karibuni na kusisitiza kuwa Baghad itakabiliana vilivyo na vyanzo na wale wote wanaowaunga mkono na kuwasaidia magaidi, licha ya kuwepo matatizo na vizingizi katika mapambano dhidi ya ugaidi.
Haidar al Abadi Waziri Mkuu wa Iraq ameashiria kuwepo vyanzo ambavyo kama alivyosema vinawasaidia magaidi na kueleza kuwa na hapa ninamnukuu,"sisi tunahafamu vyema kwamba kuna vyanzo na watu wanaounga mkono ugaidi; na kwa sababu hiyo tutazidisha mapambano na vita vyetu dhidi ya magaidi na waungaji mkono wao," mwisho wa kunukuu.
Al Abadi ameyatamka hayo katika ujumbe alioutoa kwa jamii ya kimataifa Jumapili usiku. Al Abadi amebainisha kuwa magaidi hawana uwezo wa kukabiliana moja kwa moja na vikosi vya Iraq na kwamba jibu la Baghdad kwa vitendo viovu na vya kinyama vya magaidi na maadui wa taifa la Iraq litakuwa kali kama ilivyothibitishwa na nchi hiyo huko Ramadi, Tikrit na Faluja.
Waziri Mkuu wa Iraq ameyasema hayo kufuatia mashambulizi ya umwagaji damu yaliyotekelezwa na kundii la kigaidi la Daesh Jumapili wiki hii katika eneo lenye msongamano mkubwa watu na la manunuzi huko Baghdad; ambapo watu 175 waliuawa na wengine 180 kujeruhiwa huku wote wakiwa ni raia wa kawaida.
Wachambuzi wa mambo na maafisa wa Iraq wameyataja mashambulizi hayo ya kigaidi kuwa ni ulipizaji kisasi wa Daesh mkabala na pigo walilopata hivi karibuni huko Faluja hususan kuangamizwa msafara mkubwa wa kundi hilo la kigaidi uliokuwa ukiondoka Iraq. Katika shambulio hilo dhidi ya Daesh, magari 450 na mamia ya magaidi hao waliangamizwa huko kusini mwa Faluja. Waziri Mkuu wa Iraq ametahadharisha kuhusu uwezekano wa kutekelezwa mashambulizi ya kulipiza kisasi ya magaidi na waungaji mkono wao baada ya kujiri tukio hilo la kupambana na ugaidi nchini humo ambalo linatajwa kuwa la aina yake kutokea Iraq katika miaka ya hivi karibuni.
Pamoja na hayo yote Matamshi ya Jumapili usiku ya Waziri Mkuu wa Iraq kuhusu kukabiliana Baghdad na waungaji mkono wa makundi ya kigaidi yanayofanya hujuma huko Iraq yanadhihirisha kuwa vita dhidi ya wale wote wanaowaunga mkono magaidi kifedha na kilojistiki vina umuhimu sawa kabisa na kuendesha mapambano ya moja kwa moja dhidi ya magaidi. Sababu hiyo imemfanya Waziri Mkuu Haidary al Abadi aiombe jamii ya kimataifa kushirikiana bega kwa bega na Iraq dhidi ya magaidi na waungaji mkono wao.
Pamoja na kuwa serikali ya Iraq mara hii imetoa kipaumbele na kuzingatia kwa pamoja suala la kupambana na ugaidi na waungaji mkono wake, lakini nukta hii haipasi kusahahaulika kwamba vita dhidi ya magaidi vinaweza pia kuchunguzwa kwa upande wa ndani. Hii ni kwa sababu kuondoka vikosi vya Marekani huko Iraq, kuliikasirisha Washington kutokana na kudhoofika nafasi yake katika eneo na huko Iraq; na hivyo nchi hiyo kufanya kila njama ili kuandaa uwanja wa kuibua baadhi ya mivutano na mizozo ya kikamadhehebu nchini humo. Katika fremu hiyo inaonekana kuwa mapambano ya pamoja ya serikali ya Iraq dhidi ya ugaidi, kuwaarifisha waungaji mkono wa kifedha na kilojitistiki wa magaidi katika taasisi za kimataifa na wakati huo huo Baghdad kuendesha vita vya kiadiolojia dhidi ya fikra za utumiaji mabavu na kupenda machafuko, kunaweza kufanikisha jitihada za Baghdad za kutokomeza ugaidi khususan wa kundi la kitakfiri la Daesh.