Iran na Saudia zataka vita dhidi ya Gaza visitishwe mara moja
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran na mwenzake wa Saudi Arabia wamesisitizia udharura wa kusimamishwa mapigano katika Ukanda wa Gaza haraka iwezekanavyo, sambamba na kutaka kufikishwa misaada ya kibinadamu katika eneo hilo la Palestina lililo chini ya mzingiro.
Hossein Amir-Abdollahian na Mwanamfalme Faisal bin Farhan wametoa mwito huo leo Jumatano katika mkutano wao mjini Geneva, Uswisi na kusisitiza kuwa, jamii ya kimataifa inapasa kuchukua hatua za kusimamisha uhalifu wa kivita Gaza.
Hossein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameeleza bayana kuwa, ulimwengu wa Kiislamu unapasa kuongeza mashinikizo dhidi ya utawala wa Kizayuni na serikali ya Marekani hadi pale usitishaji vita wa kudumu katika eneo la Gaza utakapoanza kutekelezwa.
Bin Farhan amesema Riyadh na Tehran zina msimamo mmoja kuhusu suala la Palestina na kutaka kukomeshwa uvamizi na jinai za kutisha za Israel dhidi ya Wapalestina wa Gaza.
"Tuna mtazamo unaofanana juu ya kuliunga mkono taifa la Palestina, kusimamishwa vita mara moja na kutumwa misaada ya kibinadamu ya dharura huko Gaza, na tutaendelea na jitihada hizi," ameongeza Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudia.
Aidha mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Saudia amelaani kimya na mapuuza ya jamii ya kimataifa na kubainisha kuwa, "Undumakuwili juu ya vita vya Gaza haukubaliki."

Zaidi ya Wapalestina 18,400 wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto wameuawa kikatili wakati wa vita vya mauaji ya halaiki ambavyo Israel ilivianzisha tarehe 7 Oktoba, kufuatia operesheni iliyofanywa na makundi ya muqawama ya Gaza iliyopewa jina la Operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa.
Kadhalika, Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Saudi Arabia wamejadili masuala ya pande mbili na kieneo, hususan hali inayoendelea katika ardhi za Wapalestina zinazokaliwa kwa mabavu.
Abdollahian amesema anaridhishwa na mwenendo wa kuimarika zaidi uhusiano wa Tehran na Riyadh na kubainisha kuwa, Iran na Saudia ni nchi mbili muhimu na zenye ushawishi katika eneo la Asia Magharibi.