Ugaidi hauna mipaka
Katika siku za hivi karibuni walimwengu wameshuhudia mlolongo wa hujuma za kigaidi kuanzia Lebanon mpaka Iraq na kisha Syria, Bangladesh, baadhi ya maeneo ya Afrika na hata nchini Saudi Arabia.
Masaa machache tu baada ya kutokea shambulio la kigaidi mjini Baghdad Jumapili usiku ambapo mamia ya watu waliuawa na kujeruhiwa, Jumatatu usiku walimwengu walipata habari ya kutokea mashambulio mengine ya kigaidi nchini Saudi Arabia. Bahram Qasemi, msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameziliwaza familia za wahanga wa matukio hayo ya kigaidi na kusema kuwa, kama ambavyo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetangaza mara chungu nzima kwamba, inalaani ugaidi wa aina yoyote ile na mahala popote utakapotokea, kuna haja pia kwa nchi zote kulifuatalia suala hilo na kutafuta chanzo chake.
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisema pia wakati akilaani shambulio la kigaidi la Bangladesh kwamba, matukio hayo yanathibitisha kwamba, ugaidi hautambui mipaka, utaifa, dini wala jiografia na kwamba, ili kupambana nao kuna haja ya kuweko ushirikiano wa pamoja wa nchi zote.
Ugaidi ambao leo unachomoza katika Mashariki ya Kati, kwa miaka mingi ilikuwa ukiilenga Iran.
Ugaidi unaoshuhudiwa hii leo hususan katika Mashariki ya Kati ni natija ya siasa za kindumakuwili za madola ya Magharibi katika kukabiliana na makundi ya kigaidi.
Ukweli wa mambo ni kuwa, Marekani imekuwa ikiwahadaa walimwengu ambapo badala ya kupambana na ugaidi imekuwa ikiuunga mkono.
Katika hali ambayo, ugaidi umekuwa ukisababisha hasara na maafa yasiyofidika ambapo jiwe lake la msingi liliwekwa na tukio la Septemba 11 mwaka 2001; lakini Marekani imetoa maana na fasili yake yake yenyewe ya ugaidi ambapo imekuwa ikiugawa ugaidi katika makundi mawili ya ugaidi mzuri na mbaya.
Nchi za Magharibi na baadhi ya nchi za Kiarabu katika Mashariki ya Kati ikiwemo Saudi Arabia na Uturuki zimekuwa zikiwasaidia magaidi kwa kuwapatia fedha na suhula na hata silaha ili makundi hayo ya kigaidi yaweze kuajiri mamluki kutoka mataifa mbalimbali. Hatua hizo maana yake ni kuunga mkono ugaidi. Hii leo matukio hayo yanaendelea kukakaririwa huku waungaji mkono wa magaidi wakiutumia ugaidi na vitendo vya kufurutu mpaka kama wenzo wa kuzusha hitilafu baina ya Uislamu na ulimwengu wa Magharibi.
Katika mazingira kama haya ambapo nchi za ukanda wa magharibi mwa Asia zimekumbwa na mvurugiko wa kisiasa na mashinikizo yanayotokana na vita na ugaidi, madola makubwa yanayopenda kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine yamelitumbukiza katika machafuko eneo hilo kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi.
Katika ujumbe wake muhimu wa Novemba mwaka jana akiwahutubu vijana wa nchi za Magharibi, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alilitaja shambulio la kigaidi la Ufaransa kuwa ni tukio chungu mno.
Kwa hakika mitazamo na misimamo ya wazi ya Iran inaonesha kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imekuwa ikilitambua suala la kupambana na ugaidi kuwa ni jambo la dharura na hali iko namna hivyo hata katika kipindi cha sasa; kwani ugaidi hauna mipaka na kupambana nao kunahitajia ushirikiano wa nchi zote.