Ansarullah: Marekani haijafikia malengo yake kwa kuishambulia Yemen
Mkuu wa shirika la habari la Harakati ya Ansarullah ya Yemen amesema mashambulizi ya Marekani dhidi ya vituo vya makombora ya harakati hiyo ya muqawama hayajafanikiwa, na kwamba Washington imeshindwa kufikia malengo yake kwa hujuma hizo.
Nasreddin Amer ameiambia kanali ya televisheni ya al-Araby leo Jumamosi kwamba, vikosi vya Yemen vina uwezo wa kushambulia meli na manowari za kijeshi za Marekani na utawala haramu wa Israel.
Ameeleza bayana kuwa, meli nyingine zote isipokuwa za US na Israel zipo salama kupita katika maji ya Bahari Nyekundu, na kusisitiza kuwa hazitalengwa na kushambuliwa na vikosi vya Yemen.
Amer amesema vikosi vya Yemen vitajibu uvamizi na uchokozi wa US na Uingereza dhidi ya Yemen kupitia mashambulizi ya ardhini na baharini na kwamba, Washington ndiyo imekanyaga sheria za kimataifa kwa kuikingia kifua Israel katika hujuma za utawala huo haramu dhidi ya Wapalestina wa Gaza.
Afisa huyo wa Ansarullah ya Yemen amesisitiza kuwa, msimamo wa watu wa Yemen katika kuwaunga mkono na kuwasaidia watu wa Palestina dhidi ya uchokozi wa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel na Marekani hautabadilika
Katika upande mwingine, Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Ansarullah ya Yemen imeeleza katika taarifa kwamba hujuma za hivi karibuni za Marekani na Uingereza dhidi ya nchi hiyo hazitapita bila jibu. Mashambulizi dhidi ya Yemen yamefanywa baada ya vikosi vya nchi hiyo kuzishambulia meli kadhaa zinazomilikiwa na utawala wa Kizayuni wa Israel katika Bahari Nyekundu, ikiwa ni hatua ya kuwaunga mkono Wapalestina wa Gaza
Kikosi cha anga cha US usiku wa kuamkia jana Ijumaa na leo Jumamosi kilishambulia kwa kutumia makombora 100 zaidi ya maeneo 60 katika makao 16 ya Jeshi la taifa la Yemen, ambapo kutokana na mashambulio hayo watu watano wameuawa na wengine sita wamejeruhiwa.
Wakati huo huo, wanafunzi wa Vyuo Vikuu vya Iran usiku wa kuamkia jana walifanya maandamano nje ya ubalozi wa Uingereza hapa Tehran, kulaani hatua ya Marekani na Uingereza ya kushambulia ardhi ya Yemen.
Wanachuo hao wa Kiirani waliokuwa wamebeba bendera za Ansarullah na za makundi mengine ya muqawama wametangaza uungaji mkono wao kwa Harakati ya Ansarullah wakisisitiza kuwa, kundi hilo lina haki ya kujibu mapigo. Aidha wamewapongeza wananchi wa Yemen kwa kuendelea kuwahami ndugu zao wa Palestina.