Matokeo ya mwisho ya uchaguzi wa Pakistan
Tume ya Uchaguzi ya Pakistani imetangaza matokeo ya mwisho ya uchaguzi wa bunge nchini humo, na wagombea huru wenye mfungamano na chama cha Tehreek-e-Insaf cha Imran Khan wamenyakua viti 101.
Katika uchaguzi wa Bunge wa Pakistani uliofanyika Februari 8, Chama cha Muslim League Nawaz kimepata viti 75 na Pakistan People's Party kimepata viti 54.
Hii ni mara ya kwanza katika historia ya kisiasa ya Pakistan ambapo wagombea huru, ambao wengi wao wanaungwa mkono na Waziri Mkuu wa zamani wa nchi hiyo Imran Khan, wanachomoza na kushinda viti vingi zaidi katika bunge.
Pamoja na hayo, hakuna hata kambi moja kati ya kambi tatu iliyofanikiwa kushinda nusu ya viti vya Bunge +1 kati ya viti 266 vya Bunge ili iweze kuunda serikali. Kwa muktadha huo serikali ijayo ya Pakistan itakuwa muungano.
Kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi ya Pakistan, ikiwa hakuna chama kitakachopata viti vingi vya asilimia 50 jumlisha kiti kimoja katika uchaguzi wa Bunge, basi chama kilichoshinda au chama chenye viti vingi lazima kiunde muungano ili kiweze kuunda serikali.
Ama hii kwamba, wagombea binafsi watasalia kuwa watiifu kwa Tehreek-e-Insaf bungeni ni suala muhimu ambalo litaonyesha uzito na nafasi ya vyama vya siasa katika Bunge lijalo nchini Pakistan.
Ikiwa wawakilishi huru walioshinda uchaguzi wataendelea kuwa waaminifu kwa Tehreek-e-Insaf, chama hiki kinaweza kuunda serikali ya mseto kwa kufanya mazungumzo na vyama vingine. "Abbas Khatak", mtaalamu wa masuala ya kimataifa, anasema kuhusiana na hili: "Kura ya wananchi kwa wagombea huru wanaohusishwa na Tehreek-e-Insaf inaonyesha kukubalika kwa kaulimbiu zake, hasa kuhusu uhuru katika sera za kigeni na kupiga vita umaskini.
Fauka ya hayo, kuachwa nyuma vyama viwili vya Muslim League Nawaz na Pakistan People's Party baada ya kutimuliwa vumbi na wagombea huru wanaohusishwa na Tehreek-e-Insaf katika uchaguzi, kunachukuliwa kuwa tukio kubwa na la kushangaza katika matukio ya kisiasa ya Pakistan.
Katika hali ambayo, Mohammad Nawaz Sharif alikuwa ameanzisha juhudi za kila upande kupata wadhifa wa Waziri Mkuu na hata inasemekana kuwa alishafikia ia makubaliano na Chama cha Pakistan People kwa minajili ya kuunda serikali ya mseto, matokeo ya sasa ya uchaguzi wa Bunge yanaweza kuvuruga mahesabu yake yote na kusambaratisha ndoto zake za kuiongoza tena Pakistan akiwa Waziri Mkuu. Katika mazingiira haya nafasi ya jeshi pia ni muhimu sana katika kuamua hatima na mustakabali wa kisiasa wa Pakistan.
Hii ina maana kwamba, ni muhimu namna chama cha Tehreek-e-Insaf kitakavyochanga karata na wawakilishi wake huru katika uga wa kisiasa wa Pakistan na pengine kitahitaji kushirikiana na jeshi la nchi hiyo.
Ikiwa ushirikiano huu hautafanywa ipasavyo, uwezekano kwamba hali ya kisiasa ya Pakistan itakabiliwa na hali tete si jambo lililo mbali.
Hii ni kutokana na kuwa, kulingana na imani ya baadhi ya duru nchini Pakistan, chaguo la jeshi lilikuwa chama cha la Muslim League na pengine uwaziri mkuu wa Muhammad Nawar Sharif.
Ikumbukwe kuwa, kuondolewa kwa uungwaji mkono wa jeshi kwa Imran Khan wakati alipokuwa Waziri Mkuu, kulisababisha Bunge kumpigia kura ya kutokuwa na imani naye, na hivi sasa bado yuko gerezani. Kwa msingi huo, bila ya kupata himaya ya jeshi, Chama cha Tahrebak Insaf kitakuwa na kibarua kigumu cha kuunda serikali ya mesto nchini Pakistan.
Hii ina maana kwamba, uzoefu wa vyama tawala kama vile Muslim League Nawaz na Tehreek-e-Insaf unaonyesha kwamba, kushinda uchaguzi wa bunge si sharti la lazima na la kutosha kwa ajili ya kushika hatamu za uongozi nchini Pakistan na kuwa na uongozi bora.