Iran yaitaka ICJ isitishe ukaliaji wa mabavu wa ardhi za Palestina
(last modified Fri, 23 Feb 2024 03:31:30 GMT )
Feb 23, 2024 03:31 UTC
  • Iran yaitaka ICJ isitishe ukaliaji wa mabavu wa ardhi za Palestina

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayeshughulikia masuala ya sheria na kimataifa ameitaka Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) iulazimisha utawala wa Kizayuni uhitimishe sera yake ya kukalia kwa mabavu ardhi za Palestina.

Reza Najafi alitoa mwito huo jana Alkhamisi katika kikao kinachojadili kadhia ya uvamizi wa utawala wa Kizayuni wa Israel na kukaliwa kwa mabavu ardhi ya Palestina na kuongeza kuwa, utawala ghasibu wa Israel unakanyaga haki ya Wapalestina ya kujiamulia mustakabali wao kwa kutumia njia mbali mbali, kama kuendelea kukalia kwa mabavu ardhi za Wapalestina kwa muda mrefu.

Najafi ameeleza kuwa, njama nyingine zinazotumiwa na Wazayuni kukwamisha uundaji wa taifa huru la Palestina ni kubadilisha muundo wa kujiografia na kidemografia wa Palestina, kubadilisha hali ya mji wa Quds Tukufu na kupuuza haki ya Wapalestina ya kuwa na mamlaka kamili na ya kudumu kwa rasilimali zao. 

Mwandiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran ameiambia ICJ kuwa, ukatili na mashambulizi ya utawala wa Israel Ukanda wa Gaza ni kinyume cha sheria za kimataifa, na kwamba ushauri wa kisheria utakaotolewa na ICJ utaandaa mazingira ya kuokoa maisha ya maenelfu ya wanawake na watoto wadogo wasio na hatia wa eneo hilo.

Waziri Najafi katika Mahakama ya ICJ

Najafi ameongeza kuwa, uamuzi wa mahakama hiyo ya Umoja wa Mataifa yenye makao yake mjini The Hague nchini Uholanzi utakuwa na mchango athirifu kwa juhudi za muda mrefu za Wapalestina za kupata haki zao halali na kujiamulia mustakabali wao.

Kabla ya hapo, wawakilishi wa Afrika Kusini, Saudi Arabia na Algeria katika Mahakama ya ICJ walisisitiza kuwa, uvamizi na mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza yanatisha zaidi kuliko mfumo wa ubaguzi wa rangi wa apartheid, na kutaka kuhitimishwa ukaliaji wa mabavu wa ardhi za Palestina.

Siku ya Jumatatu, ICJ ilianza kusikiliza shauri la kuamua kuhusu uhalali wa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel wa kuzivamia na kuzikalia kwa mabavu ardhi za Palestina.

Shauri hilo liliwasilishwa mahakamani hapo kufuatia ombi la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) la mwishoni mwa mwaka 2022. Nchi zaidi ya 50 zitaendelea kuwasilisha hoja zao katika mahakama ya ICJ hadi Februari 26. 

Tags