Muqawama walitia hasara kubwa jeshi la Israel Gaza na Lebanon
Makundi ya muqawama yamelisababishia hasara kubwa jeshi la Israel katika Ukanda wa Gaza, wakati huu ambapo utawala huo wa Kizayuni unandeleza mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wasio na ulinzi wa eneo hilo lililo chini ya mzingiro.
Press TV imeripoti kuwa, wanajihadi wa Brigedi za Mashahidi wa al-Aqsa, ambao ni muungano wa makundi ya muqawama wenye makao yake makuu katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, leo Jumatatu wamefanya operesheni 14 dhidi ya vikosi vya Israel na kuvisababishia hasara kubwa ya vifo na majeruhi.
Aidha wanajihadi wa Brigedi za Izzuddin al-Qassam, tawi la kijeshi la Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS wamefanya operesheni kadhaa kwa kutumia droni dhidi ya kambi ya kijeshi ya Israel mashariki mwa mji wa Beit Hanoun, kaskazini mwa Gaza.
Wakati huo huo, Harakati ya Hizbullah ya Lebanon imejibu jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya Ukanda wa Gaza kwa kushambulia kwa makombora kituo cha kijeshi ya Israel kaskazini mwa ardhi za Palestina zilizopachikwa jina bandia la Israel.
Televisheni ya al-Manar imeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, wamamuqawama wa kundi hilo wamewashambulia askari wa Israel katika eneo la Barka Risha kwa makombora ya Burkan, saa chache baada ya kuyamininia makombora maeneo ya Wazayuni katika mashamba ya Shebaa.
Kadhalika wamamuqawama wa Palestina wametangaza habari ya kudhibitiwa ndege isiyo na rubani ya Israel (droni), ikiwa ni kuendelea kujibu jinai za Wazayuni dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.
Taarifa ya Brigedi za Quds, tawi la kijeshi la harakati ya muqawama ya Jihad Islami ya Palestina imesema kuwa, droni hiyo ya kijasusi ya utawala wa Kizayuni imetwaliwa na wanajihadi kaskazini mwa kambi ya wakimbizi ya Bureij, katikati ya Ukanda wa Gaza.
Makundi ya muqawama yanasisitiza kuwa, kadiri utawala wa Kizayuni wa Israel unavyozidisha mashambulio dhidi ya taifa la Palestina na Ukanda wa Gaza, ndivyo hasara inavyozidi kuongezeka kwa utawala huo pandikizi.