Yemen yashambulia meli za Marekani na Israel katika Bahari ya Hindi
(last modified Sat, 16 Mar 2024 07:38:53 GMT )
Mar 16, 2024 07:38 UTC
  • Yemen yashambulia meli za Marekani na Israel katika Bahari ya Hindi

Vikosi vya Jeshi la Yemen vimetangaza habari ya kupanua operesheni zao kwa kuzishambulia meli za Marekani na utawala haramu wa Israel katika maji ya Bahari ya Hindi.

Brigedia Jenerali Yahya Saree, Msemaji wa jeshi la taifa la Yemen alisema hayo jana Ijumaa akihutubu umati mkubwa uliojiotokeza kushiriki maandamano ya kila wiki ya kuwaunga mkono wananchi madhulumu wa Palestina na kueleza kuwa, vikosi vya jeshi hilo vimezishambulia meli tatu za Marekani na Israel katika Bahari ya Hindi.

Brigedia Jenerali Saree amebainisha kuwa, jeshi la Yemen limezishambulia meli za Marekani na Israel katika Bahari ya Hindi katika kuwaunga mkono wananchi madhulumu wa Palestina na kujibu uvamizi wa Marekani na Uingereza dhidi ya Yemen.

Saree amesema: Vikosi vyetu vimefanya operesheni tatu dhidi ya meli tatu za Marekani na Israel katika Bahari ya Hindi kwa kutumia makombora na ndege zisizo na rubani (droni), na operesheni hizo zimefanikiwa pakubwa.

Brigedia Jenerali Yahya Saree

Shambulio hilo limejiri siku moja baada ya Kiongozi wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen, Sayyid Abdul Malik Al-Houthi kusema askari wa jeshi la nchi hiyo wataendelea na operesheni zao za kujibu mapigo dhidi ya meli za kibiashara zenye uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel, kwa kuzizuia meli hizo kupita hata kwenye eneo la maji ya Bahari ya Hindi na Rasi ya Tumaini Jema.

Viongozi wa Ansarullah ya Yemen wamesisitiza kuwa operesheni hizo zitaendelea maadamu hujuma na mzingiro dhidi ya Gaza unaendelea. Marekani na Uingereza zilianza kuishambulia Yemen mwezi Januari ili kuizuia nchi hiyo kuzilenga meli za Israel zinazobeba silaha na vifaa kwa ajili ya mashambulizi katika Ukanda wa Ghaza uliozingirwa.