Watu wenye silaha waua abiria 11 kusini magharibi mwa Pakistan
Apr 14, 2024 02:30 UTC
Watu wenye silaha wameua abiria wasiopungua 11 katika matukio mawili tofauti yaliyojiri kusini magharibi mwa Pakistan.
Naibu Kamishna wa Polisi Nushki Habibullah Mosakhel amewaambia waandishi wa habari kuwa, matukio hayo yamejiri katika wilaya ya mbali ya jimbo la Baluchistan kusini magharibi mwa nchi, wakati watu wenye silaha wasiojulikana walipofunga barabara kuu inayounganisha Pakistan na Iran na kuwaua abiria hao.
Kwa mujibu wa Mosakhel, katika tukio la kwanza, watu hao wenye silaha walilizuia gari moja na kuwateka nyara abiria tisa wengi wao wakiwa vibarua, baada ya kuangalia utambulisho wao na kwenda nao kwenye eneo la milima ya jirani. Watu wote hao tisa waliotekwa nyara baadaye walipigwa risasi na kuuawa na miili yao ikatupwa karibu na daraja.
Imeelezwa kuwa, marehemu hao wanatokea kaskazini-magharibi mwa Punjab, jimbo kubwa zaidi nchini Pakistan.
Katika tukio jengine tofauti, watu wenye silaha wanaosadikiwa kuwa wa kundi lilelile lilioua vibarua, walilifyatulia risasi basi la abiria ambalo halikusimama na kusababisha vifo vya watu wawili na wengine watano kujeruhiwa.
Hadi sasa hakuna kundi ambalo limedai kuhusika na mashambulizi hayo, ingawa waasi wa kabila la Baluchi wamekuwa wakiwalenga wafanyakazi kutoka sehemu nyingine za Pakistan, hasa Punjab.
Mnamo Oktoba mwaka jana, watu wenye silaha waliwaua wafanyakazi sita wa ujenzi na kuwajeruhi wengine wawili katika shambulio la kabla ya alfajiri kwenye kambi yao karibu na wilaya ya Turbat.
Kwa miongo kadhaa, Wabaluchi wanaotaka kujitenga wamekuwa wakipigania jimbo la Baluchistan lenye utajiri wa rasilimali lijitenge na Pakistan.
Waziri Mkuu Shehbaz Sharif amelaani mauaji hayo, na kuapa kwamba vikosi vya usalama vitang'oa mizizi ya "zimwi" la ugaidi.
Katika taarifa yake, Shehbaz Sharif ameviagiza vyombo vya usalama kutumia suhula zote kuhakikisha wahusika wanafikishwa mbele ya mkono wa sheria.../
Tags