OIC yalaani 'maandamano ya bendera' ya Israel ya kusherehekea kuivamia Quds Mashariki
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i112610-oic_yalaani_'maandamano_ya_bendera'_ya_israel_ya_kusherehekea_kuivamia_quds_mashariki
Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) imelaani 'maandamano ya bendera' ya utawala wa Kizayuni wa Israel yaliyofanyika jana Jumatano Baitul Muqaddas Mashariki kwa mnasaba wa kumbukumbu ya kuuvamia na kuanza kuukalia kwa mabavu mji huo mwaka 1967.
(last modified 2026-05-13T14:18:38+00:00 )
Jun 06, 2024 03:19 UTC
  • OIC yalaani 'maandamano ya bendera' ya Israel ya kusherehekea kuivamia Quds Mashariki

Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) imelaani 'maandamano ya bendera' ya utawala wa Kizayuni wa Israel yaliyofanyika jana Jumatano Baitul Muqaddas Mashariki kwa mnasaba wa kumbukumbu ya kuuvamia na kuanza kuukalia kwa mabavu mji huo mwaka 1967.

Kwa mujibu wa mashuhuda, makundi ya mrengo wa kulia ya Kizayuni jana yalifanya maandamano hayo kupitia Mji Mkongwe wa Quds (Jerusalem), huku walowezi wa mrengo wa kulia wakikusanyika na kufanya uchochezi katika eneo la Waislamu la mji huo.
 
Mashuhuda hao wameeleza kuwa Wazayuni wa mrengo wa kulia waliwashambulia wakazi Wapalestina katika Mji wa Kale wa Baitul Muqaddas wakati wa maandamano hayo.
 
Katika taarifa yake, OIC imelaani vikali uvamizi uliofanywa na utawala ghasibu wa Kizayuni "katika eneo la Msikiti wa Al-Aqsa huko Baitul Muqaddas Mashariki na kuwaruhusu walowezi wa Kizayuni kuandaa maandamano ya uchochezi" katika mji huo.
 
Taarifa ya Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu imesisitiza: "Quds (Jerusalem) ni mji mkuu wa Nchi ya Palestina na ni sehemu muhimu ya maeneo ya Palestina yaliyokaliwa kwa mabavu mnamo mwaka 1967".

OIC imeongezea katika taarifa yake kwa kusema: "tunapinga hatua au maamuzi yoyote yanayolenga kulazimisha mamlaka ya Israel juu ya mji huu na maeneo yake matakatifu kwa sababu yanatambulika kuwa ni kinyume cha sheria".

 
Wapalestina wanasisitiza kuwa Baitul Muqaddas Mashariki ni mji mkuu wa inayotarajiwa kuwa nchi yao huru, wakinukuu maazimio ya kimataifa ambayo hayatambui ukaliaji wa mabavu wa mji huo unaofanywa na utawala wa Kizayun wa Israel tokea mwaka 1967 au kuunganishwa kwake na Baitul Muqaddas Magharibi mwaka 1981.
 
Hali ya wasiwasi imetanda katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu, ikiwa ni pamoja na Quds Mashariki, tangu Israel ilipoanzisha mashambulizi ya kinyama na mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Ghaza baada ya operesheni ya kulipiza kisasi ya Kimbunga cha Al-Aqsa iliyotekelezwa na harakati ya Hamas Oktoba 7, 2023.
 
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Palestina ya Ukingo wa Magharibi, hadi sasa Wapalestina wasiopungua 527 wameuawa shahidi na wengine karibu 5,000 wamejeruhiwa kutokana na mashambulio ya jeshi la Israel katika eneo hilo linalokaliwa kwa mabavu.../